Na Brian Okoth
Miss Universe Nigeria, Chidimma Adetshina, ametawazwa mshindi wa pili katika shindano la Miss Universe 2024 nchini Mexico.
Adetshina alikuja nyuma ya Victoria Kjær Theilvig wa Denmark, ambaye alitawazwa mshindi Jumapili, Novemba 17. Takriban washiriki 130 walishiriki.
Mshindi wa tatu alikuwa Maria Fernanda Beltran wa Mexico, huku Muthaithai Suchata Chuangsri na Ileana Marquez Pedroza wa Venezuela wakiingia kwenye tano bora.
Adetshina wa Nigeria mwenye umri wa miaka 23, Sakhile Dube mwenye umri wa miaka 28 wa Zimbabwe na Logina Salah wa Misri mwenye umri wa miaka 34 wameingia kwenye 30 bora.
Wanawake wenye umri wa zaidi ya miaka 28 wanaruhusiwa kushindana
Kuanzia 2024, wanawake wenye umri wa zaidi ya miaka 28 wanaruhusiwa kushiriki katika mashindano.
Mnamo 2023, Miss Universe iliruhusu wanawake wajawazito, akina mama na walioolewa kushiriki katika shindano hilo.
Adetshina alikaribia sana kushinda taji la 2024 siku ya Jumapili, huku Theilvig wa Denmark mwenye umri wa miaka 21 ndiye mshiriki pekee aliyeorodheshwa juu zaidi.
Adetshina, kwa hivyo, alitawazwa Miss Universe Africa na Oceania.
'Huwawezesha wanawake kutokata tamaa kamwe'
Oceania ni kundi la nchi 14, zikiwemo Australia, New Zealand, na Fiji.
Miss Universe Nigeria ilisema katika taarifa siku ya Jumapili kwamba onyesho la kuvutia la Adetshina "huwapa wanawake vijana uwezo wa kutimiza ndoto zao na kamwe wasikate tamaa."
Baada ya kutangazwa mshindi wa kwanza, Adetshina alisema katika mahojiano kuwa hatarajii kufika katika nafasi tano za juu.
"Si kwamba nina mashaka (kujihusu), lakini nahisi mashindano yalikuwa magumu sana, lakini ninafurahi sana kwamba nilifanikiwa, si kwa ajili yangu tu, bali kwa Nigeria kwa sababu waliniunga mkono. Lakini si kwa Nigeria pekee, lakini kwa Afrika,” alisema.
Safari isio rahisi
Safari ya Adetshina hadi taji la mshindi wa pili la Miss Universe imekuwa si rahisi.
Hapo awali alikuwa mshiriki wa Miss Afrika Kusini 2024, na alikuwa miongoni mwa waliofika fainali 13 kabla ya mambo kuharibika.
Mapema Agosti, serikali ya Afrika Kusini ilianzisha uchunguzi kuhusu uraia wake baada ya madai kuibuka kwamba mama yake, ambaye ana asili ya Msumbiji, alidaiwa kuiba maelezo ya utambulisho wa mwanamke mwingine wa Afrika Kusini ili kumsajili Adetshina wakati wa kuzaliwa mwaka 2001.
Maelezo ya awali yalionyesha Adetshina alizaliwa na kukulia katika eneo la Soweto la Johannesburg, na baadaye alihamia Cape Town.
Kujitoa katika shindano la Afrika Kusini
Baba yake Adetshina ni raia wa Nigeria.
Katikati ya mzozo wa uraia, Adetshina alitangaza kujiondoa kwenye shindano la Miss Afrika Kusini 2024 mnamo Agosti 8, akitaja wasiwasi juu ya "usalama na ustawi wa familia yake."
Mshindi hatimaye , Mia Le Roux, alitawazwa mnamo Agosti 10.
Le Roux mwenye umri wa miaka 29 alijiondoa kwenye shindano la hivi majuzi la Miss Universe huko Mexico kwa sababu za kiafya.
Ushindi wa taji la Miss Universe Nigeria
Baada ya Adetshina kujiondoa katika shindano la Miss Afrika Kusini, Miss Universe Nigeria alimwalika kushiriki katika shindano sawia la nchi hiyo.
Adetshina alikubali mwaliko huo, na alitawazwa Miss Universe Nigeria 2024 mnamo Agosti 31 kutoka kwa kundi la washiriki 25.
Katika shindano la Nigeria aliwakilisha jimbo la kaskazini-mashariki la Taraba.
Kama mshindi wa pili, anarudi nyumbani na zawadi ya pesa ambayo haijabainishwa, na ufikiaji wa anuwai ya bidhaa za urembo.
Uraia wa Afrika Kusini 'kufutwa'
Mnamo Oktoba 29, mamlaka ya Afrika Kusini ilisema Adetshina na mamake watapoteza uraia wao wa Afrika Kusini, na pia kufunguliwa mashitaka kwa madai ya kupata hati za uraia "haramu".
Mshindi wa Miss Universe, Theilvig wa Denmark, atapokea mshahara wa kila mwaka wa dola za Marekani 250,000, safari zilizopangwa kwa zaidi ya nchi 30, na usambazaji wa mwaka mmoja wa vipodozi vya Miss Universe, anasa na mapambo.
Katika shindano la Miss Universe, majaji hutafuta kujiamini, uhalisi, uaminifu, uwezo wa kuonyesha neema chini ya shinikizo, na pia uwezo wa kueleza nia ya mtu.
Mashabiki wanaweza pia kupiga kura ili kupata washiriki katika fainali, lakini majaji hatimaye huamua mshindi.