Watu wenye silaha wameripotiwa kuwaua zaidi ya watu 40 katika shambulizi dhidi ya jamii ya wachimba madini katika jimbo la Plateau la kati nchini Nigeria, vyombo vya habari vya ndani viliripoti Jumanne.
Wakaazi walisema shambulio hilo lilitokea Jumatatu jioni katika kijiji cha mbali cha Zurak katika wilaya ya Bashar eneo la serikali ya mtaa wa Wase, kulingana na ripoti ya chapisho la The Daily Trust.
Sahpi'i Sambo, kiongozi wa vijana katika eneo hilo alisema watu wenye silaha waliokuwa wakiendesha pikipiki walifika katika jamii mwendo wa saa kumi na moja jioni kwa saa za huko na kuanza kufyatua risasi kiholela.
Sambo alisema zaidi ya watu 40 waliuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa.
Aliongeza kuwa wakaazi walikimbilia jamii jirani kwa usalama.
Jeshi la Nigeria bado halijatoa tamko kuhusiana na tukio hilo.
Mashambulizi ya watu wenye silaha na utekaji nyara ni jambo la kawaida sana nchini Nigeria ambapo matukio ya mapigano baina ya jamii pia yamekithiri.