Na
Khalida Khan
Hapa Uingereza, tumepitia uuaji wa kikatili dhidi ya Waislamu, lakini huwezi kujua. Ukisoma matangazo ya vyombo vya habari ya wiki chache zilizopita, hutafikiri kwamba chuki dhidi ya Waislamu ndiyo chanzo cha ghasia hizo nchini kote.
Toka kuanze kwa machafuki hiyo, kila mtu hapa anazungumza kuhusu ghasia za "ubaguzi wa rangi" au "vurugu." Makala ya hivi majuzi ya BBC kuhusu jinsi waziri mkuu wetu anavyopaswa kushughulikia "mizizi" ya ghasia hizo ilishindwa kutaja chuki dhidi ya Waislamu hata mara moja.
Na siku ya Ijumaa, kamati ya Umoja wa Mataifa iliitaka Uingereza kupitisha hatua za kuzuia matamshi ya chuki na matamshi ya chuki dhidi ya wageni, lakini pia ilishindwa kutaja chuki dhidi ya Uislamu.
Hata hivyo, waandamanaji hao hawakulenga makanisa, masinagogi, mahekalu ya Kihindu au gurdwara za Sikh, lakini walilenga misikiti, na katika kesi moja hata makaburi ya Waislamu. Kichochezi cha ghasia dhidi ya Waislamu huko Southport kilitokana na taarifa potovu zilizoratibiwa mtandaoni, kwamba mhalifu aliyetekeleza mauaji ya wasichana wadogo kwenye darasa la ngoma alikuwa Mwislamu na mtafuta hifadhi.
Walengwa wa waandamanaji hao walikuwa Waislamu, bila shaka yoyote, ambayo iliongezeka na kujumuisha watu wa rangi ya kahawia na Weusi.
Hakuna kinachotokea hivi hivi tu. Ubaguzi wa kihistoria dhidi ya Uislamu, pamoja na miongo kadhaa ya mijadala isiyozuilika dhidi ya Uislamu katika nchi hii katika kila ngazi ya jamii, ilihitaji tu cheche kuwasha moto.
Southport ilikuwa cheche hiyo.
Kupuuza chuki dhidi ya Waislamu
Wakati baadhi ya wanasiasa na ripoti za vyombo vya habari awali zilikiri kwamba Waislamu ndio walilengwa na mashambulizi ya mwezi uliopita, ukweli huu sasa unapuuzwa.
Uingereza ina sheria zinazoruhusu mahakama kushtaki uhalifu unaochochewa na chuki za kidini, lakini hadi sasa, inaonekana waandamanaji wameshtakiwa kwa makosa "yaliyochochewa na ubaguzi wa rangi", sio "kuchochewa na dini", ambayo tena inadharau uchochezi dhidi ya Uislamu.
Ikiwa ninalohofia ni sahihi, inaonekana kuna uwezekano mkubwa kwamba serikali ya Chama cha ''Labour'' haitashughulikia chiki dhidi ya Uislamu kabisa au kwa njia yoyote ya maana katika uchunguzi wowote unaoendelea.
Kufanya hivyo kutamaanisha kufikiria upya kabisa na kuhuisha upya hali ilivyo pamoja na kuhusisha kufanya mabadiliko makubwa ya kitaasisi - katika sekta nzima ya umma, ikiwa ni pamoja na mfumo wa Haki ya Jinai, uelewa wa huduma za ustawi wa mahitaji ya Waislamu, na polisi kushughulikia chuki dhidi ya Uislamu kama uhalifu.
Tumefikaje hapa? Daima kumekuwa na kukana kuwepo kwa chuki dhidi ya Uislamu katika mazungumzo ya kawaida ya Waingereza. Badala yake, vyombo vya habari vya kawaida, sekta ya umma na serikali zinaonekana kupendelea kuangalia tatizo kana kwamba ni tatizo la ubaguzi wa rangi.
Aina mbili za chuki
Wengi hawataelewa kwa nini ni muhimu kwamba ubaguzi dhidi ya Uislamu uwe tofauti na ubaguzi wa rangi. Wacha nielezee.
Ili kupata suluhisho bora kwa shida, lazima utambue sababu sahihi za msingi. Huwezi kuweka pamoja chuki dhidi ya Uislamu na ubaguzi wa rangi, kwani ni aina mbili tofauti za chuki. Kuna haja ya kutumia mbinu tofaut ili kupatikane kwa matokeo chanya.
Chuki dhidi ya Uislamu ni dhana potofu iliyokita kwenye mizizi na woga uliokithiri kwa Waislamu katika fikra ya Wamagharibi, ambayo husababisha unyanyasaji na ubaguzi.
Kwa zaidi ya miaka elfu moja hadi leo, Ulaya imekuwa katika hali ya msuguano kwa njia nyingi na Uislamu. Fikiria miaka 800 ya Waislamu wa Uhispania, Vita vya Msalaba na Uthmaniyya huko Uropa.
Migogoro hii imesababisha baadhi ya wanahistoria na wanasiasa wa Ulaya kuwaona Waislamu kama 'wanaume wajinga', 'wapotovu wa ngono', 'wakandamizaji wa wanawake', 'washenzi' na sasa 'magaidi', watu ambao wanatishia nchi za Magharibi.
Haya yote yanaonekana katika historia ya Uropa, fasihi, sanaa, vyombo vya habari na Hollywood (tazama filamu ya hali halisi ya Jack Shaheen Reel Bad Arabs).
Wakati ubongo wako ukiwa umechangiwa na kuogopa na kuuchukia Uislamu na Waislamu, haichukui muda mrefu kwa fikra za chuki dhidi ya Uislamu kukita mizizi na kubadilika kuwa tabia ya ubaguzi, unyanyasaji na mashambulizi.
Hii ni historia ya 'Islamophobia'. Sio kuhusu rangi, bali chuki ya muda mrefu dhidi ya Uislamu na Waislamu.
Ubaguzi wa rangi, kwa upande mwingine, unatokana na ubaguzi kutokana na rangi ya ngozi na asili ya kabila. Ina historia yake pia.
Inatokana na nadharia za Uropa kuhusu jamii, huku wenye rangi nyeupe wakijiona kuwa bora zaidi na wa rangi za nyeusi na kahawia wamedharauliwa. Aina zote hizi mbili za chuki zinatumika kuhalalisha utumwa na ukoloni.
Wakati mwingine chuki dhidi ya Uislamu na ubaguzi wa rangi hupishana, lakini bado ni lazima ichukuliwe kama aina tofauti za chuki, ili kuwe na masuluhisho madhubuti kwa zote mbili.
Nchini Uingereza, vuguvugu la kupinga ubaguzi wa rangi ambalo liliendelezwa katika miaka ya 1950 kushughulikia ubaguzi wa rangi halikuhusika na dini na lilihusu tu rangi ya ngozi. Kwa hakika, ubaguzi wa dini au wa ubaguzi wa kidini uliondolewa kimakusudi kutoka kwa vuguvugu hilo kwani "lilikuwa na mgawanyiko mkubwa," kama nilivyoambiwa kwenye kikao cha mafunzo na Ambalavaner Sivanandan mwenyewe, mwanaharakati maarufu wa kupinga ubaguzi wa rangi.
Harakati nchini Uingereza zilianza wakati wahamiaji wapya wa rangi na imani tofauti walifika Uingereza baada ya vita, ambapo walikabiliwa na unyanyasaji wa ubaguzi wa rangi, mashambulizi, ghasia na mauaji yaliyochochewa na rangi.
Kufikia miaka ya 1970 na 1980, jumuiya mbalimbali ziliungana kwa sababu sote tulikuwa tukilengwa juu ya rangi ya ngozi yetu. Lakini hata hivyo, ubaguzi dhidi ya Uislamu ulikuwepo kama ungekuwa na macho ya kuona, kama vile mauaji ya mwanafunzi Mwislamu katika shule yenye misimamo ya chuki dhidi ya Uislamu, na mauaji ya mfungwa kijana na maofisa wa gereza wenye chuki dhidi ya Uislamu.
Matukio haya ya chuki dhidi ya Uislamu hayakuwahi kuainishwa kama hivyo, kwa sababu watunga sera waliona tu ubaguzi wa rangi, si chuki ya kidini.
Usawa wa rangi uliwaacha Waislamu nje
Kufuatia ghasia za ubaguzi wa rangi za mwanzoni mwa miaka ya 1980, serikali iliagiza sekta ya umma kuanzisha mipango ya usawa wa rangi. Kama afisa wa uhusiano wa rangi, niligundua hivi karibuni kuungana dhidi ya ubaguzi wa rangi ilikuwa jambo moja, lakini kulazimisha "lebo za rangi na utambulisho" kwetu kama Weusi na Wa-asia, na kisha kuzitumia kutoa huduma kwa jamii tofauti za kidini na kitamaduni katika sekta ya umma ilikuwa kitu kingine.
Kwa hakika, ilikuwa ni balaa kwa Waislamu. Hakika, Sheria ya Mahusiano ya Rangi ya 1976 ililinda tu vikundi vya rangi, na Waislamu kuwa wa makabila mengi na kikundi cha imani, hawakulindwa.
Nilianza kuona serikali na sekta ya umma kutokuwa na uelewa kamili hata wa kuwepo kwa Waislamu; tulikuwa hawatuoni.
Waislamu kwa muda mrefu wamekuwa, na bado ni, mojawapo ya jumuiya zisizo na uwezo wa kijamii na kiuchumi na kiafya nchini Uingereza, na hiyo ni kwa sababu walionekana kutoonekana kwa kutokuwepo; ama kutopata huduma, au huduma zinazotolewa hazikuwa na hisia au zisizofaa.
Kwa mfano, ilipokuja suala la kulea na kuasili, watoto wa Kiislamu waliwekwa katika makundi ya jamii moja, badala ya wale wa imani moja. Kwa hivyo mtoto wa Kiislamu wa Nigeria angewekwa pamoja na Wakristo wa Kiafrika-Caribbean, na mtoto wa Kiislamu wa Pakistani kuwekwa pamoja na Wahindu wa Kihindi.
Kwetu sisi kama Waislamu, kipaumbele chetu ni kwamba watoto wa Kiislamu wanapaswa kuwekwa katika familia za Kiislamu, hata kama kuweka pamoja kikabila haiwezekani kila mara.
Nchini Uingereza, Sensa haikuwa na swali kuhusu dini hadi 2001, hivyo ilikuwa vigumu kuhesabu ubaguzi ambao Waislamu walikabiliana nao.
Kushawishi mabadiliko
Mnamo 1985, nilianzisha Jumuiya ya An-Nisa, ili kufanya kazi kwa ajili ya ustawi wa familia za Kiislamu na kukuza ufahamu wa masuala niliyoyabainisha.
Baada ya miaka mingi ya ushawishi na kampeni, kulikuwa na mafanikio madogo na mafanikio makubwa, ikiwa ni pamoja na Sheria ya Usawa ya 2010 ambayo hatimaye ilijumuisha "dini na imani" kama tabaka lililolindwa. Sasa tulikuwa na sheria inayoharamisha uhalifu wa chuki uliokithiri kidini na uchochezi wa chuki ya kidini.
Kazi yetu kuhusu programu za kijamii kama vile kutoa ushauri na nasaha kwa jamii za Kiislamu pia ilionyesha kuwa mipango ya kidini ilielekea kuwa na matokeo bora ya kijamii na kiuchumi.
Hata hivyo pamoja na hatua hizi kubwa zinazoendelea, huku Waislamu wengi sasa wakiwa katika siasa na sekta ya umma, chuki dhidi ya Uislamu imeongezeka, kama inavyoshuhudiwa katika uuaji wa kikatili dhidi ya Waislamu.
Hiyo ni kwa sababu bado wanalichukulila kama ubaguzi wa rangi.
Waislamu wanatakiwa kujielimisha
Kikwazo kibaya zaidi cha kushughulikiwa kwa chuki dhidi ya Uislamu ni Waislamu wenyewe.
Viongozi wa jumuiya ya Kiislamu, ambao hawaelewi jinsi Uislamu unavyofanya kazi na wao wenyewe wameratibiwa kuamini kwamba chuki dhidi ya Uislamu ni sawa na ubaguzi wa rangi, hawaipi serikali na watunga sera jambo linloweza kufanywa na kutekelezwa ili kukabiliana na kweli chuki dhidi ya Uislamu.
Ni chuki dhidi ya Uislamu ya kitaasisi ambayo inawaathiri Waislamu kwa undani zaidi. Kwa vile hawana matarajio kutoka kwa sekta ya umma ya kupatiwa imani inayohitajika sana na huduma za kitamaduni zinazofaa, hawaelewi kwamba ukosefu huu wa upatikanaji wa huduma hizo unasababisha moja kwa moja kutengwa kwao kijamii.
Badala yake, wamezoea kuona kila kitu kuweka katika kategoria ya "ubaguzi wa rangi" na kukubali hali kama ilivyo.
Pigo kubwa zaidi kwa mapambano lilikuwa Kundi la Wabunge wa Vyama Vyote (APPG) juu ya ufafanuzi wa Waislamu wa Uingereza wa Islamophobia kama "aina ya ubaguzi wa rangi" mnamo 2017, ambayo ilirudisha nyuma mafanikio yote tuliyopata na kukubalika na kukuzwa na wanasiasa Waislamu na viongozi.
Vita vyetu vyote vya kuondoa chuki dhidi ya Uislamu kutoka kwa ubaguzi wa rangi vilibadilishwa kwa ufafanuzi huo.
Baada ya maandamano
Baada ya ghasia hizi za hivi majuzi zaidi dhidi ya Waislamu, ninahofia kwamba nchi yangu itarudi katika hali ya kuziona tu jumuiya za wachache kama makundi ya "watu wenye rangi" na kutuchukulia sote kana kwamba ni kundi moja la watu wa jinsia moja.
Maana yake ni kwamba iwapo hatua zozote zitachukuliwa na serikali kubaini na kushughulikia chanzo cha ghasia hizo, zitaangaliwa kwa misingi ya rangi. Chuki dhidi ya Uislamu utawekwa chini ya ubaguzi wa rangi na maazimio hayatakuwa makubwa katika upeo wao na mikakati iliyobuniwa.
Lakini kuibua maneno yale yale ya kikabila na mikakati ambayo imewashinda Waislamu wa Uingereza kwa miongo kadhaa haitafanya kazi.
Sina matumaini kwamba sera zozote za kitaasisi zitatolewa ili kukabiliana na chuki dhidi ya Uislamu katika maeneo yanayotendeka, ikiwa ni pamoja na mitandao ya kijamii, mazingira ya kisiasa na taasisi, kuruhusu Waislamu kuwa watu wa hali ya chini.
Lakini Sheria ya Usawa inatupa zana za kushughulikia chuki dhidi ya Uislamu kwa jinsi tunavyotendewa na kupokea huduma zetu, tunahitaji kuitumia ipasavyo.
Sasa tuna sheria za kushughulikia uhalifu wa chuki dhidi ya Waislamu, lakini lazima tushinikize polisi na Mfumo wa Haki ya Jinai kuzitumia. Hii ni fursa ya mabadiliko.
Miongo kadhaa iliyopita, kama tungechukua hatua zinazofaa za kukabiliana na chuki dhidi ya Uislamu na kama tungewekeza katika jumuiya ya kiraia ya Kiislamu yenye uwezo mkubwa wa kushughulikia mahitaji yetu ya pande nyingi na yenye uwezo wa kututetea kwa ustadi - tusingekuwa na hali tuliyo nayo sasa.
Mwandishi, Khalida Khan ni mwanzilishi mwenza na Mkurugenzi wa Jumuiya ya An-Nisa yenye makao yake Uingereza, shirika lenye makao yake makuu nchini Uingereza linalofanya kazi katika kujenga jumuiya ya kiraia yenye nguvu ya Kiislamu. Kama mwanaharakati, mpiga kampeni na mwandishi wa masuala ya Kiislamu, Khan mara kwa mara anaangazia kuhusu masuala ya imani, utoaji wa huduma na sekta ya hiari ya Waislamu na jamii na ni mshauri wa vyombo vya habari na watafiti. Khan pia alibuni neno ‘Institutional Islamophobia’ ili kubainisha ubaguzi dhidi ya Waislamu katika sera na tabia.
Kanusho: Maoni yaliyotolewa na mwandishi hayawakilishi lazima maoni, mitazamo na sera za uhariri za TRT Afrika.