Meli huzama kwani kuvuka ni hatari hasa katika njia hii / Picha: AFP

Boti lililobeba wahamiaji 280 lilitua kwenye Visiwa vya Canary nchini Uhispania, baada ya kuvuka mojawapo ya njia hatari zaidi za uhamiaji Katika Bahari ya Atlantic.

Wahamiaji hao ndio idadi kubwa zaidi kufika kwa mashua moja kwenye visiwa, kikundi cha uokoaji kilisema.

Wahamiaji hao, ambao wanajumuisha wanaume 278 wakiwemo wavulana 10 pamoja na wanawake wawili, ni wa asili ya "kusini mwa Jangwa la Sahara", kulingana na waokoaji waliowapokea walipowasili.

Ripoti za vyombo vya habari vya Uhispania zilisema kuwa meli hiyo ilifika bandari la La Restinga kwenye kisiwa kidogo cha El Hierro kilomita 450 (maili 285) kutoka pwani ya Afrika.

Wahamiaji 14,976 waliwasili Canaries kati ya Januari 1 na Septemba 30, ikiwa ni ongezeko la asilimia 19.8 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mnamo 2022, kulingana na takwimu za hivi karibuni kutoka wizara ya mambo ya ndani ya Uhispania.

Tangu mwanzoni mwa mwaka huu, wahamiaji 140 wamefariki au kutoweka kupitia njia hii, kulingana na takwimu kutoka Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) kutoka mapema septemba.

Shirika lisilo la Kiserikali uhispania Caminando Fronteras, ambalo, tofauti na IOM linategemea simu za dharura kutoka kwa wale walio baharini au jamaa zao, inakadiria kuwa wahamiaji 778 walikufa au kutoweka kwenye njia hii ya uhamiaji katika nusu ya kwanza ya mwaka.

AFP