Waziri wa ulinzi wa Uhispania Margarita Robles, alisema siku ya Jumamosi kwamba vita vya Israel dhidi ya Gaza ni "mauaji ya kimbari ya kikweli", huku uhusiano kati ya Tel Aviv na Madrid ukizidi kuwa mbaya kufuatia uamuzi wa Uhispania wa kulitambua taifa la Palestina.
Reuters haikuweza mara moja kuwafikia maafisa wa Israel ili kutoa maoni yao siku ya Jumamosi.
Israeli imekanusha vikali shutuma zilizotolewa dhidi yake na Afrika Kusini, katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ), kwamba inafanya mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina, ikisema inaendesha vita dhidi ya kundi la Hamas.
Matamshi ya Waziri wa Ulinzi wa Uhispania Margarita Robles, katika mahojiano na televisheni ya taifa ya TVE, yaliunga mkono maoni ya Naibu Waziri Mkuu wa Uhispania Yolanda Diaz, ambaye mapema wiki hii pia alielezea vita dhidi ya Gaza kuwa mauaji ya halaiki.
"Hatuwezi kupuuza kile kinachotokea Gaza, ambayo ni mauaji ya kimbari ya kikweli," Robles alisema katika mahojiano, ambapo pia alijadili uvamizi wa Urusi nchini Ukraine na migogoro barani Afrika.
Pia alisema kutambua kwa Madrid Palestina sio hatua dhidi ya Israeli, akiongeza kuwa iliundwa kusaidia "kukomesha ghasia huko Gaza".
"Hii sio dhidi ya mtu yeyote, hii sio dhidi ya serikali ya Israeli, hii sio dhidi ya Waisraeli, ambao ni watu tunaowaheshimu," alisema.
Israeli imewauwa karibu Wapalestina 36,000 huko Gaza, kulingana na maafisa wa afya wa Palestina huko Gaza, na kuharibu sehemu kubwa ya eneo hilo.
Uhispania, pamoja na Ireland na Norway, ilitangaza wiki hii kuwa itatambua taifa la Palestina mnamo Mei 28, na kusababisha jibu la hasira kutoka kwa Israeli, ambayo ilisema ni sawa na "tuzo kwa ugaidi" na kuwaita mabalozi wake kutoka miji mikuu hayo mitatu.
Majaji katika mahakama ya juu ya Umoja wa Mataifa ICJ, siku ya Ijumaa wameiamuru Israeli kusitisha mara moja mashambulizi yake ya kijeshi huko Rafah, katika uamuzi wa dharura wa kihistoria katika kesi iliyowasilishwa na Afrika Kusini inayoishutumu Israeli kwa mauaji ya halaiki.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uhispania Jose Manuel Albares, alisema siku ya Jumamosi kuwa Israeli lazima itii uamuzi wa mahakama.
"Hatua za tahadhari zilizotolewa ma mahakama ya ICJ , ikiwa ni pamoja na kusitisha mashambulizi ya Israeli huko Rafah, ni za lazima. Tunataka yatekelezwe," alisema kupitia mtandao wa kijamii wa X.
Afrika Kusini imeishutumu Israeil kwa kukiuka Mkataba wa Mauaji ya Kimbari ya mwaka 1948.
Israeli inakanusha shutuma hizo, ikisema kuwa inajilinda na kupambana na Hamas baada ya shambulio la Oktoba 7, ambapo watu 1,200 waliuawa na zaidi ya 250 walichukuliwa mateka.
Siku ya Jumatano, Waziri Mkuu wa Uhispania Pedro Sanchez alisema, kwamba ikiwa mataifa zaidi yatatambua taifa la Palestina itaongeza shinikizo la kimataifa la kusitishwa kwa mapigano kati ya Israeli na Hamas.