Na Ahmet Yusuf Ozdemir
Kupinduliwa kwa Bashar al Assad na mabadiliko ya serikali nchini Syria ndani ya wiki mbili za upanuzi wa upinzani kutoka Idlib na Daraa kulikuja kama mshtuko kwa wengi. Kuondolewa kwa Assad kulikuja baada ya miaka 13 ya vita vya wenyewe kwa wenyewe. Lakini kwa kweli ni matokeo ya mchakato ulioanza miaka 100 iliyopita.
Katika kuadhimisha miaka mitano ya ghasia za Syria mnamo Machi 2016, wachambuzi walidai kuwa mapinduzi hayo yameshindwa. Mapinduzi ya nchi za Kiarabu yamefeli, haswa huko Syria.
Mienendo ya kimapinduzi hutulazimisha kufikiria zaidi ya uchanganuzi wa kisiasa wa kijiografia, unaozingatia jukumu la watendaji wa kikanda na kimataifa. Kwa upande wa Syria, hili lilifikiwa na uthabiti wa upinzani wa Syria, ambao waliweka kumbukumbu zao safi kuhusu ukatili wa utawala wa al Assad, hata huko ughaibuni.
Mienendo ya kijamii na kisiasa ya mapinduzi ya hivi karibuni ya Desemba 8 nchini Syria yatachambuliwa kwa kina zaidi katika miongo ijayo kutoka pande tofauti. Ikiwa tutakuwa na bahati ya kutosha, tutasoma habari kutoka kwa pande zote zinazohusika kuhusu jinsi michakato ya mapinduzi iliafikiwa, na majibu ya familia ya Assad.
Walakini, jambo moja linapaswa kuwa wazi kwa sasa: mapinduzi ya Syria lazima yachambuliwe kama mwendelezo wa mchakato ambao haukuanza mnamo 2011, lakini ule unaorudi nyuma hadi wakati wa Uasi wa Syria wa kupinga ukoloni dhidi ya Wafaransa mnamo 1925.
Mapinduzi ni muundo, sio tukio. Mapinduzi ni jambo la kizazi ambapo kila kizazi kipya hujifunza kutokana na uzoefu wa mababu zao. Mapinduzi yana macho, masikio na akili ya aina yake. Muda muafaka ukifika, unaweza kuwashwa na kumshika kila mtu kwa mshangao. Hiki ndicho kilichotokea Syria.
Kizazi cha mapinduzi
Hii inaweza kuonekana kama maneno ya kupita kiasi, lakini mifumo ya kisasa ya kisiasa duniani kote haijaona mabadiliko kama hayo ambayo yamefanyika nchini Syria.
Ndio, kupinduliwa kwa Assad kulikuja baada ya dhoruba ya Mapinduzi ya Nchi za Waarabu kufika Damascus mnamo 2011 na kutimia mnamo 2024. Hata hivyo, haiwezi kulinganishwa na mabadiliko ya haraka ya utawala yaliyotokea katika maeneo mengine ambayo yaliathiriwa na mawimbi ya maandamano, kama vile Tunisia na Misri.
Zine El Abidine ben Ali alitawala Tunisia kati ya 1987 na 2011. Hosni Mubarak alitawala Misri kati ya 1981 na 2011. Utawala wa Ben Ali ulifikia kikomo baada ya kampeni ya siku 28 ya upinzani wa raia. Mubarak alilazimika kujiuzulu baada ya siku 18 za ukaidi wa raia.
Wakati wimbi la Mapinduzi ya Nchi za Kiarabu lilipofikia Damascus mwaka 2011, kasi na kumbukumbu bado zilikuwa mpya kutokana na majaribio ya awali ya kumpindua dikteta.
Hili lilidhihirika zaidi baada ya milango ya gereza la Sednaya hatimaye kufunguliwa mwezi uliopita. Mfano halisi: Rubani wa Jeshi la Wanahewa la Syria Ragheed Al-Tatari, ambaye alifungwa gerezani akiwa na umri wa miaka 27 mnamo 1980 kwa kukataa maagizo ya jeshi ya kuwalipua raia huko Hama na kuachiliwa baada ya miaka 43. Kizazi kilichoanzisha hatua za awali za mapinduzi kilitoka kwa tamaduni, kazi, na miji tofauti.
Wito wa mabadiliko daima umekuwa uleule, mwepesi lakini wa kudumu, kwa miaka 100 iliyopita, kuanzia 1925 hadi 2025.
Wakati Wasyria walipoasi mfumo wa mamlaka ya Ufaransa, madai yao yaliibua kauli mbiu maarufu ya Mapinduzi ya Ufaransa: Uhuru, Usawa, na Udugu.
Tangu siku zake za mwanzo, kwa mfano wa Syria, kwa upande mwingine, kauli mbiu maarufu ilianzishwa na serikali na wafuasi wake: " Kubaki kwa Assad au tunachoma nchi." Kwa kweli, ndivyo ilivyokuwa baada ya miaka 13 ya vita vya wenyewe kwa wenyewe. Miaka 13, miezi 8, na siku 23, kuwa sahihi.
Licha ya mzozo wa kisiasa na kutokua na maendeleo ya kisiasa Libya na Yemen, tunaweza kusema kwa Mapinduzi ya Syria, na Mapinduzi ya Nchi za Kiarabu, kwa kiasi kikubwa yameisha baada ya kuanguka kwa Bashar al Assad.
Serikali mpya ya Syria inajaribu kuunda upya mfumo wa kisiasa, kiuchumi na kijeshi wa nchi hiyo kutoka chini kwenda juu, jambo ambalo si rahisi.
Ili kuiweka katika uhalisia, ni lazima kuzingatia ukweli kwamba Syria imekuwa na machafuko ya kisiasa tangu kuanzishwa kwake. Kati ya 1922 na 1970 kwa mfano, kulikuwa na mabadiliko 16 ya mamlaka, saba kati yao kupitia mapinduzi ya kijeshi.
Kabla ya utawala wa familia ya Assad kuchukua madaraka, viongozi wengi walidumu kwa miezi 18 pekee.
Kasi ya mapinduzi
Mapinduzi ya Nchi za Kiarabu huenda kuwa yameisha, lakini machafuko katika Mashariki ya Kati yanaendelea.
Baada ya mwaka mmoja na nusu ya mauaji ya kimbari huko Gaza na Israeli, mapinduzi ya Syria yametukumbusha ukweli kwamba mabadiliko ya kisiasa yanawezekana.
Je, kuondolewa kwa Assad kunaweza kusababisha mchakato wa pili wa Mapinduzi ya Nchi za Kiarabu? Hili ni swali linapaswa kuzingatiwa. Lakini angalau kwa wakati huu, serikali ya mpito ya Syria na mipango yake ya sera za kigeni haijaonyesha jaribio lolote la "kusafirisha" mapinduzi yake katika eneo hilo.
Mapinduzi yanadai mahitaji ya msingi ya binadamu. Kwa maana fulani ni uasi dhidi ya msisitizo wa utawala wa zamani wa kujaribu kuelekeza mtazamo wa umma kwenye "picha kubwa" au "maadui wa kigeni na wa ndani," na badala yake kuandika historia tukufu yao wenyewe.
Syria ya utawala wa Assad ulikuwa mfano mkuu wa hili. Akizungumza katika Mkutano wa Kilele wa Kiislamu wa Kiarabu, wiki tatu kabla ya kupinduliwa, Bashar al Assad hakukwepa kuionyesha Syria kama bingwa wa kadhia ya Palestina.
Wakati kwa upande mwingine, baba yake Hafez ndiye aliyesaidia kuigawanwa muqawama wa Palestina kwa kulenga juhudi zake huko Lebanon.
Kwa hakika, wakati Jamhuri ya Syria inaweza kuwa imepata uhuru wakati wanajeshi wa mwisho wa Ufaransa waliosalia walipoondoka Aprili 17, 1946, watu wa Syria walipata uhuru wao wa kweli wakati Bashar al Assad alikimbia kutoka Damascus kwenda Moscow.
Mwandishi, Ahmet Yusuf Ozdemir, ni Profesa Msaidizi wa Sayansi ya Siasa na Idara ya Uhusiano wa Kimataifa katika Chuo Kikuu cha Ibn Haldun.
Maoni yaliyotolewa na mwandishi hayaakisi maoni na sera za uhariri za TRT Afrika.