Marekani iko katika hali ya tahadhari na kujiandaa kwa shambulio linaloweza kufanywa na Iran linalolenga mali ya Israel au Marekani katika eneo hilo kujibu mashambulizi ya Israel dhidi ya ubalozi wa Iran nchini Syria, afisa wa Marekani alisema.
"Hakika tuko katika hali ya tahadhari," afisa huyo alisema katika kuthibitisha ripoti ya CNN ambayo ilisema shambulio linaweza kutokea wiki ijayo.
Ndege za kivita za Israel zilishambulia ubalozi wa Iran mjini Damascus siku ya Jumatatu katika shambulizi lililomuua kamanda wa jeshi la Iran na kuashiria ongezeko kubwa la vita vya Israel na mahasimu wake wa kikanda.
Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Iran limesema kuwa washauri saba wa kijeshi wa Iran walifariki katika shambulizi hilo akiwemo Mohammad Reza Zahedi, kamanda mkuu katika Kikosi chake cha Quds, ambacho ni kikosi maalumu cha kijeshi.
Iran imesema inahifadhi haki "ya kuchukua jibu madhubuti."
Rais wa Marekani Joe Biden alizungumzia tishio hilo kutoka kwa Iran katika mazungumzo ya simu siku ya Alhamisi na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu.
"Marekani imepata taarifa za kijasusi kwamba Iran inapanga mashambulizi ya kulipiza kisasi ambayo yatajumuisha kundi la ndege zisizo na rubani za Shahed na makombora ya masafa marefu," CBS News iliripoti Ijumaa.
"Maafisa wanasema muda na lengo haujulikani, lakini jibu sawia kwa shambulio la Damascus litakuwa kukipiga kituo cha kidiplomasia cha Israel. Shambulio hilo huenda likatokea kati ya sasa na mwisho wa Ramadhani wiki ijayo," tovuti ya habari ya Marekani iliripoti.
Iran yaiambia Marekani kujitenga
Iran ilisema iliitaka Marekani "kujitenga" wakati ikijibu mashambulizi ya Israel dhidi ya ubalozi wake.
"Katika ujumbe ulioandikwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inauonya uongozi wa Marekani kutoburuzwa katika mtego wa Netanyahu kwa Marekani: Kaa pembeni ili usije kuumia," Mohammad Jamshidi, naibu mkuu wa wafanyakazi wa rais wa Iran katika masuala ya kisiasa aliandika katika mtanao wa X.
"Kwa kujibu Marekani iliitaka Iran kutolenga vituo vya Marekani."
Wakati huo huo, mkuu wa Hezbollah Hassan Nasrallah amelitaja shambulio la Israel dhidi ya ujumbe wa kidiplomasia wa Iran kuwa ni hatua ya mabadiliko na kusema kulipiza kisasi kwa Tehran "hakuepukiki."
Vyombo vya habari vya Israel viliripoti kwamba mamlaka mjini Tel Aviv wanafikiria kufungua makazi ya hifadhi ya dharura huku kukiwa na vitisho vya Iran vya kulipiza kisasi.
Jeshi la Israel limeamua kuwaita wanajeshi wa akiba kwenye safu yake ya ulinzi ya anga, katika hatua iliyoelezwa na vyombo vya habari vya ndani kama hatua ya tahadhari dhidi ya uwezekano wa mashambulizi ya kulipiza kisasi kutoka kwa Iran.