"Kutiririka hadi nchini Syria sio tu hatari; tayari imeanza," amesema Geir Pedersen, mjumbe wa UN kwa Syria. / Picha: Reuters

Mgogoro kati ya Israel na Palestina unazidi kusambaa nchini Syria, ukichochewa na kuongezeka kwa ukosefu wa utulivu, ghasia na ukosefu wa suluhisho la kisiasa la mzozo huo wa miaka 12, mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa nchini humo amesema.

Geir Pedersen ameliambia Baraza la Usalama kwamba, kuhusiana na ghasia za mzozo wa Syria, watu wa Syria sasa wanakabiliwa na "matarajio ya kutisha ya uwezekano mkubwa wa kuongezeka" kufuatia mashambulizi ya Hamas ya Oktoba 7 dhidi ya Israel na hatua inayoendelea ya kulipiza kisasi.

"Kuenea hadi nchini Syria sio hatari tu; tayari imeanza," mjumbe wa Umoja wa Mataifa kwa Syria alisema.

Pedersen aliashiria mashambulizi ya anga yanayohusishwa na Israel kuvipiga viwanja vya ndege vya Syria huko Aleppo na Damascus mara kadhaa, na hatua ya Marekani ya kulipiza kisasi dhidi ya kile ilichosema ni mashambulizi mengi yaliyolenga vikosi vyake "na makundi ambayo inadai yanaungwa mkono na Iran, ikiwa ni pia ndani ya Syria. "

Huku eneo hilo "likiwa katika hali ya hatari na hali ya wasiwasi," alisema, " Uchochezi unaendelea kwenye mzozo ambao tayari ulikuwa umeanza kuwaka" nchini Syria, ambayo ilikuwa ikishuhudia kuongezeka kwa ghasia hata kabla ya Oktoba 7.

Pedersen aliongeza kuwa idadi ya Wasyria waliouawa, kujeruhiwa na kukimbia makazi yao iko juu zaidi tangu 2020, akitaja kuongezeka kwa mashambulizi katika maeneo yanayodhibitiwa na serikali ya Syria, ikiwa ni pamoja na shambulio kwenye sherehe za kuhitimu katika chuo cha kijeshi huko Homs ambalo halijulikani lilitekelezwa na nani.

Marekani, Urusi walaumiana

Balozi wa Marekani Linda Thomas-Greenfield alishutumu "makundi ya kigaidi," baadhi yanayoungwa mkono na Syria na Iran, kwa kutishia kupanua mgogoro wa Gaza "na kutumia eneo la Syria kupanga na kuanzisha mashambulizi dhidi ya Israeli."

Aidha, aliishutumu Syria kwa kuruhusu Iran na "makundi ya kigaidi" kutumia viwanja vyake vya ndege vya kimataifa kwa madhumuni ya kijeshi.

"Marekani imewaonya wahusika wote kutochukua fursa ya hali ya Gaza kupanua au kuongeza mzozo," Thomas-Greenfield alisema.

Balozi wa Urusi Vassily Nebenzia, mshirika wa karibu wa Syria, alishutumu vikosi vya Israel kwa kushambulia maeneo nchini Syria, yakiwemo viwanja vya ndege vya kiraia, na kuyataja mashambulizi ya Marekani nchini humo kuwa ni "vitendo visivyo halali" na "ukiukaji mkubwa wa uhuru wa Syria."

Aidha, alidai kuwa maslahi ya kiuchumi ya Marekani na kujihusisha "katika uvujaji wa nafaka na mafuta ya Syria" kumeshinda maslahi ya kisiasa.

Nebenzia alisema kuna ongezeko kubwa la mvutano katika mzozo wa Israel na Palestina na mashambulizi kama yale ya Marekani yanaweza kusababisha kuenea hadi eneo zima.

Balozi wa Iran katika Umoja wa Mataifa Amir Iravani aliishutumu Washington kwa kujaribu "kuondoa lawama kutoka kwa mhalifu hadi kwa muathiriwa."

Iravani aliliambia baraza hilo "uungaji mkono thabiti" wa Marekani kwa Israel "umeifanya kuwa sehemu ya tatizo."

Amesema Marekani na baadhi ya nchi za Magharibi zinajaribu kuipa Israel haki isiyo sahihi ya kujilinda huku ikipuuza haki ya wananchi wa Palestina ya kujitawala na kuufananisha jitihada za Palestina na ugaidi.

"Lengo kuu la Iran ni kuepusha kuongezeka kwa hali yoyote katika eneo," balozi huyo alisisitiza, na ndiyo maana imeidhinisha wito wa kimataifa ya kusitishwa mara moja kwa mapigano na misaada ya kibinadamu kwa watu wa Gaza.

TRT World