Uchomaji wa Quran nchini Uswidi ulisababisha Papa mtakatifu wa kanisa katoliki kulaani kitendo hicho Picha : AA

Nakala ya kitabu kitakatifu cha Waislamu, Quran ilichomwa moto na kutupwa mbele ya msikiti kusini-magharibi mwa Ujerumani, kundi la mwamvuli la Kituruki-Islamic Union for Religious Affairs (DITIB) limesema.

Tukio hilo lilitokea kutumia gari lililopitia mbele ya Msikiti wa Mimar Sinan katika mji wa Maulbronn, ulioko katika jimbo la Baden-Wurttemberg.

Osman Adibelli, mkurugenzi wa chama cha misikiti, alisema tukio hilo lilitokea usiku wa Jumamosi, Julai 8.

"Baada ya tukio hilo, tulipokagua picha za video ya usalama za msikiti wetu, tuliona kitu kilirushwa mbele ya msikiti kutoka kwa gari kwenye barabara kuu," alisema katika taarifa yake Jumatatu.

Malalamiko yamewasilishwa

''Waumini waliokuja kwa ajili ya swala ya asubuhi waliona Qurani iliyochomwa kwenye mlango wa msikiti," aliongeza.

Adibelli alisema wamewasilisha malalamiko ya jinai juu ya tukio hilo. "Kutokana na mwanga wa taa za gari lililokuwa likikaribia mbele ya msikiti hatujui namba ya leseni ya gari wala ni watu wangapi walihusika katika shambulio hilo."

Akionyesha masikitiko makubwa na wasiwasi juu ya shambulio hilo, Adibelli alitangaza kuwa uchunguzi umeanzishwa.

Tukio hilo limekuja kufuatia kuchomwa moto mara kadhaa au kunajisiwa nakala nyingi za Qur'ani katika nchi mbalimbali za Ulaya, ikiwa ni pamoja na kisa cha hivi karibuni zaidi cha kuchomwa moto Qur'ani mbele ya msikiti mmoja nchini Sweden, kuruhusiwa na polisi na kuibua hasira za kimataifa.

Viongozi na wanasiasa wa Kiislamu wamesisitiza kuwa unajisi wa kitabu kitakatifu na chokochoko hizo hazimo chini sheria za uhuru wa kujieleza.

Uchochezi wa wazi

Baraza la haki za kibinadamu la Umoja wa Mataifa linatazamiwa kujadili rasimu ya pendekezo kuhusu chuki za kidini kufuatia tukio hilo nchini Sweden.

Rasimu ya azimio hilo ambayo itawasilishwa kwenye baraza hilo mjini Geneva siku ya Jumanne, inapingwa na baadhi ya wawakilishi wa nchi za Magharibi.

Rasimu ya azimio iliyowasilishwa na Pakistan kwa niaba ya Jumuiya ya Nchi 57 ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) inasema, kundi hilo lilieleza kuchomwa moto kwa Qur'ani Tukufu huko Stockholm mwezi uliopita kuwa ni "kuudhi, dharau na kitendo cha wazi cha uchochezi" ambacho kinachochea chuki na ukiukaji wa haki za binadamu.

Rasimu hiyo - ambayo ililaani "vitendo vya mara kwa mara vya uchomaji wa Qur'ani Tukufu katika baadhi ya nchi za Ulaya na nyinginezo" - imezusha upinzani kutoka kwa wanadiplomasia wa Magharibi ambao wanahoji kuwa inalenga kulinda alama za kidini badala ya haki za binadamu.

TRT Afrika