Mmiliki wa nyumba huko Chicago katika jimbo la Illinois nchini Marekani alimdunga kisu mtoto wa miaka 6 hadi kufa na kumjeruhi vibaya mama yake katika shambulio ambalo huenda liliendeshwa na chuki dhidi ya Uislamu kutokana na imani ya Kiislamu ya familia hiyo na mzozo wa Israel na Palestina.
"Tumeshtushwa na kufadhaishwa kujua kwamba mwenye nyumba huko Chicago anayeonyesha maoni yake dhidi ya Uislamu na Wapalestina alivamia nyumba ya familia ya Waislamu na kuwashambulia kwa kisu na kumjeruhi mama na kumuua mtoto wake wa miaka 6, Wadea Al.Fayoume,” Baraza la Mahusiano ya Kiislamu ya Marekani (CAIR) , shirika kubwa zaidi la haki za kiraia la Waislamu nchini Marekani, lilisema kwenye X.
"Maneno ya chuki dhidi ya Uislamu na ubaguzi wa rangi dhidi ya Wapalestina unaoenezwa na wanasiasa, vyombo vya habari na mitandao ya kijamii lazima ukomeshwe," shirika hilo liliongeza.
Mashtaka ya 'Mauaji ya daraja la kwanza'
Ofisi ya mkuu wa polisi wa Wilaya ya Will baadaye ilitoa taarifa ikisema kwamba kulingana na uchunguzi wa mtaalamu wa magonjwa, mvulana huyo alidungwa kisu mara 26 katika mwili wake wote.
Mama yake mwenye umri wa miaka 32 alipata majeraha zaidi ya kumi na mbili.
Anaendelea kupata nafuu na anatarajiwa kuishi.
Mshambulizi huyo, Joseph Czuba, 71, alishtakiwa kwa mauaji ya daraja la kwanza, jaribio la mauaji ya daraja la kwanza, unyanyasaji kwa silaha mbaya na makosa mawili ya uhalifu wa chuki, ofisi ya sheriff ilisema.
Habari za kushtua na kutamausha
Rais wa Marekani Joe Biden alilaani mauaji ya mvulana huyo mwenye asili ya Palestina na Marekani.
Mke wangu Jill na mimi tulishtuka na kuudhika kusikia kuhusu mauaji ya kikatili ya mtoto wa miaka sita na jaribio la mauaji ya mama wa mtoto huyo nyumbani kwao jana huko Illinois," Biden alisema katika taarifa.
"Kitendo hiki cha kutisha cha chuki hakina nafasi nchini Marekani na kinaenda kinyume na maadili yetu ya kimsingi: uhuru kutoka kwa hofu kwa jinsi tunavyoabudu, kile tunachoamini, na utambulisho wetu," alisema.
Biden aliwataka Wamarekani kuungana dhidi ya chuki dhidi ya Uislamu kutokana na mauaji hayo.