Takriban watu 22 wameuawa na "wengi zaidi" wamejeruhiwa vibaya kupitia shambulizi la risasi katika Mji wa Lewiston, Maine Jumatano jioni, maafisa wa eneo hilo waliripoti, huku polisi wakisema kwamba mtu huyo alikuwa bado hajakamatwa.
Kansela wa jiji Robert McCarthy aliambia Shirika la Habari la CNN kwamba idadi ya vifo imeongezeka hadi kufikia 22 katika shambulio la risasi lililotokea katika uwanja wa burudani na pia angalau eneo jengine moja, mgahawa wa ndani na baa, hayo ni kulingana na vyombo vya habari.
"Uelewa wangu ni kwamba wameweza kumtambua na kupata kitambulisho cha muda wa mvamizi huyo, ninathibitisha vifo 22, na wengi, wengi zaidi kujeruhiwa," McCarthy alisema.
Polisi wa eneo hilo walisambaza picha ya mpiga risasi huyo kwenye mtandao wa Facebook akiwa amebeba kile kilichoonekana kuwa silaha ya mtindo wa 'nusu-otomatiki' ndani ya uwanja wa Bowling.
Aidha, polisi pia walitoa picha ya gari nyeupe aina ya SUV, na kuomba msaada wa umma katika kutambua gari, wakisema kuwa sehemu yake ya mbele inaweza kuwa imepakwa rangi nyeusi.
'Mvamizi bado yuko huru'
Polisi "wanachunguza matukio mawili ya wapiga risasi," idara ya polisi ya Kaunti ya Androscoggin iliandika kwenye mtandao wa Facebook.
"Tunawahimiza wafanyabiashara wote kufunga maduka yao kwa kipindi hiki huku tukiendelea na uchunguzi. Mshukiwa bado yuko huru."
Ikulu ya White House imesema kuwa rais Joe Biden amearifiwa kuhusu tukio hilo.
Na Gavana wa eneo la Maine Janet Mills alisema alikuwa " anajua tukio linaloendelea la ufwatuliaji risasi katika eneo la Lewiston."
CNN iliripoti kuwa takriban watu 50 hadi 60 walijeruhiwa katika matukio hayo, ikinukuu vyanzo vingi vya utekelezaji wa sheria, lakini ilisema haijulikani ni majeraha mangapi yaliyotokana na risasi.
Polisi na waokoaji waliripotiwa kufika katika eneo la burudani la 'Sparetime Recreation bowling alley' karibu saba na robo usiku ili kukabiliana na mvamizi huyo, na baada ya hapo kupokea ripoti ya risasi nyingine katika sehemu ya 'Schemengees Bar & Grille, kwa mujibu wa jarida la eneo hilo la Sun Journal.