Mtu mmoja amehukumiwa kifungo cha miezi 10 nchini Uingereza kwa kutoa lugha ya matusi na kumtemea mate dereva wa basi mwenye imani ya Kiislamu, mamlaka nchini humo imesema Jumanne.
Ofisi ya mashitaka ya nchini Uingereza imesema kuwa Michael Mongan mwenye miaka 39, alitoa kauli za kichochezi na kumtemea mate dereva, baada ya kukataliwa kupanda basi la abiria siku ya Julai 7, katika eneo la Hayes nchini humo.
Picha za video zilizosambaa kwa haraka mitandaoni wiki iliyopita, zilimuonesha Mongan akirudiarudia maneno ya kibaguzi yakiwemo "Gaidi wa Kiislamu" na mengineyo. Pia, alisisitiza dereva huyo ashuke kwenye basi huku akigonga kioo cha dereva huyo.
Alitambulika na kukamatwa Agosti 9, 2024.
“Matendo yake yanahusishwa na vurugu za hivi karibuni nchini Uingereza,” imesema ofisi hiyo ya mashitaka nchini humo .
Vurugu hizo zilichochewa na madai ya uongo yaliyosambaa mitandaoni kuwa mtuhumiwa aliyekamatwa Julai 29 kwa mauaji ya watoto watatu katika eneo la Southport, alikuwa ni Muislamu.
Mamlaka za nchi hiyo, zimemtambua Axel Rudakubana, mwenye miaka 17 mzaliwa wa eneo la Cardiff, huku wazazi wake wakiwa ni Wanyarwanda.
Hata hivyo, hatua hiyo haijasaidia kupunguza ghasia hizo.
Hadi kufikia Agosti 8, watu takribani 483 wamekamatwa, huku wengine 149 wakishtakiwa kwa kusababisha vurugu katika miji tofauti nchini Uingereza.