Waziri wa vita wa Israeli Benny Gantz ametangaza kujiuzulu kutoka serikali ya dharura ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu huku vita vya zaidi ya miezi saba vikiendelea huko Gaza.
"Tunajitoa kutoka serikali ya umoja kwa moyo mzito," Gantz alisema katika hotuba yake kwenye televisheni.
Gantz pia alimtaka Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kufanya uchaguzi wa mapema "haraka iwezekanavyo".
Gantz, mkuu wa zamani wa kijeshi, alijiunga na serikali ya dharura ya Netanyahu muda mfupi baada ya shambulio la Oktoba 7 la Hamas.
Kamanda mkuu wa Kijeshi amejiuzulu
Mapema leo Jeshi la Israeli limetangaza kujiuzulu kwa kamanda mkuu kufuatia shambulio la Oktoba 7.
Jeshi la Israeli limesema kuwa kamanda mmoja mkuu amejiuzulu kwa kile alichokiita kushindwa kuzuia shambulio la Oktoba 7 lililofanywa na kundi la Palestina Hamas.
"Kamanda wa Kitengo cha 143, Brigedia Jenerali Avi Rosenfeld, aliwafahamisha makamanda wake leo kuhusu nia yake ya kusitisha utumishi wake katika (jeshi la Israeli)," ilisema taarifa ya jeshi.
"Afisa huyo atamaliza kazi yake katika siku za usoni."
Rosenfeld aliandika katika barua ya kujiuzulu iliyotolewa na jeshi: "Kila mtu anapaswa kuwajibika kwa upande wake, na mimi ndiye ninahusika katika Idara ya 143."
"Mnamo Oktoba 7, nilishindwa kuwajibika kulinda jamii za Israeli ziliokuwa zikiishi kwenye mpaka na Gaza.", aliandika.