Mtazamo wa jumla unaonyesha mkutano wa Baraza la Usalama katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa, Jumanne, Novemba 19, 2024. / Picha: AP

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linatazamiwa kupigia kura mswada mwingine wa azimio la kutaka kusitishwa kwa mapigano katika eneo la Gaza huko Palestina, katika jaribio lake la hivi punde la kutoa shinikizo la kumaliza vita.

Lakini rasimu hiyo inaweza kuzuiwa na Marekani, mshirika mkuu wa Israeli.

Rasimu ya hivi punde ya azimio hilo inadai "kusitishwa kwa mapigano mara moja, bila masharti na ya kudumu" katika vita vya Israeli dhidi ya Gaza na "kuachiliwa mara moja na bila masharti kwa mateka wote."

Maneno hayo yameikasirisha Israeli na kuibua hofu ya kura ya turufu ya Marekani.

Balozi wa Israeli katika Umoja wa Mataifa Danny Danon ameyaita maandishi hayo kuwa ni ya aibu na kuongeza: "Hatuwezi kuruhusu Umoja wa Mataifa kufunga mikono ya Taifa la Israeli kuwalinda raia wake, na hatutaacha kupigana hadi tuwarudishe watu wote waliotekwa nyara na wanawake nyumbani."

"Kwetu sisi, inabidi kuwe na uhusiano kati ya usitishaji mapigano na kuachiliwa kwa mateka," alisema Robert Wood, naibu balozi wa Marekani.

"Imekuwa msimamo wetu wa kimsingi tangu mwanzo na inabaki kuwa hivyo."

Gaza 'itatuandama'

Tangu kuanza kwa vita hivyo, Baraza la Usalama limekuwa likitatizika kuzungumza kwa sauti moja, kwani Marekani ilitumia kura yake ya turufu mara kadhaa, ingawa Urusi na China pia zimetumia kura zao za turufu.

Maazimio machache ambayo Marekani iliruhusu kupitishwa kwa kujiepusha nayo yaliacha kutoa wito wa kusitishwa kwa mapigano bila masharti na ya kudumu.

Mnamo Machi, baraza hilo lilitoa wito wa kusitishwa kwa mapigano kwa muda wakati wa mwezi mtukufu kwa Waislamu wa Ramadhani, lakini bila mafanikio.

Mwezi Juni, baraza hilo liliahidi kuunga mkono mpango wa hatua mbalimbali wa Marekani wa kusitisha mapigano na kuwaachilia mateka ambao haukuenda popote.

Bila ya kutajwa kwa vikwazo

Baadhi ya wanadiplomasia wameelezea matumaini kuwa kufuatia ushindi wa Donald Trump katika uchaguzi wa Novemba 5, Rais Joe Biden anaweza kubadilika zaidi katika wiki chache ambazo amesalia madarakani.

Walifikiria uwezekano wa kurudiwa kwa matukio ya mwezi Disemba 2016 wakati rais wa wakati huo Barack Obama alipokuwa anamaliza muhula wake wa pili na baraza hilo lilipitisha azimio la kutaka kusitishwa kwa ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Israeli katika maeneo ya Wapalestina yanayokaliwa kwa mabavu, mara ya kwanza tangu 1979.

Marekani ilijizuia kutumia kura yake ya turufu katika kesi hii, kubadilisha uungaji mkono wa jadi wa Marekani kwa Israeli katika suala nyeti la makazi.

Rasimu inayopigiwa kura siku ya Jumatano pia inataka "kuingia kwa usalama na bila kuzuiliwa kwa usaidizi wa kibinadamu kwa kiwango kikubwa," ikiwa ni pamoja na kaskazini mwa Gaza iliyozingirwa, na inalaani jaribio lolote la kuwanyima Wapalestina chakula.

Ujumbe wa Palestina katika Umoja wa Mataifa umeona ya kuwa maandishi haya hayaendi mbali vya kutosha.

"Hatma ya Gaza itaandama ulimwengu kwa vizazi vijavyo," balozi Riyad Mansour alionya.

Alisema hatua pekee ya baraza hilo ni kutaka kusitishwa kwa mapigano mara moja na bila masharti kulingana na kipengele cha 7 cha katiba ya Umoja wa Mataifa. Kipengele hicho kinaruhusu baraza kuchukua hatua za kutekeleza maazimio yake, kama vile vikwazo, lakini maandishi ya hivi punde hayaangazii chaguo hilo.

TRT World