Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ametoa wito kwa vijana kutoka kote duniani kuchukua nafasi ya mbele katika kusukuma mbele suluhu za mabadiliko ya tabia nchi.
Katika ujumbe aliotoa kwa vijana kupitia mtandao wake wa X, Antonio Guterres alitambua jukumu muhimu ambalo vijana wamecheza katika kuendesha hatua za hali ya hewa na kuwataka kuongeza juhudi katika kukabiliana na hali mbaya ya mabadiliko ya tabia nchi.
''Hatua kubwa tulizopiga katika kukabiliana na ongezeko la joto duniani, imetokana kwa kiasi kikubwa na juhudi za vijana kote duniani,'' alisema Guterres.
''Nawaomba wazidishe kelele wanazopiga na kusukuma ajenda ya mabadiliko,'' aliongeza.
Guterres amethibitisha kuhudhuria kongamano kubwa la Nairobi kuanzia Septemba 4, kujadili mabadiliko ya tabia nchi na ktafutia suluhu janga hilo.
Zaidi ya wajumbe 30,000 wanatarajiwa kuwepo katika kongamano hilo wakiwemo, marais, mawaziri wa nchi mbali mbali, mashirika makubwa duniani, pamoja na vijana na wanaharakati wa mazingira.
''Nyinyi ndio taswira ya uongozi wa hali ya hewa unavyoonekana. Katika kongamano la mazingira jijini Nairobi, nitawaomba viongozi wengine wote wachukue hatua muafaka. Na nawaomba nyinyi mupaze sauti zaidi na zaidi.'' alisema Guterres katika ujumbe wake huo.