Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametangaza kuwa anatumia Kifungu cha 99 cha Mkataba wa Umoja wa Mataifa katika suala la la Gaza.
Hii inampa mamlaka ya kuitisha mkutano wa Baraza la Usalama kujadili hali inayoendelea Gaza ambayo anaiona kuwa tishio kwa amani na usalama wa kimataifa.
"Katibu Mkuu anaweza kuwasilisha kwa Baraza la Usalama suala lolote ambalo kwa maoni yake linaweza kutishia kudumisha amani na usalama wa kimataifa."
"Zaidi ya wiki nane za uhasama huko Gaza na Israel zimezua mateso ya kutisha ya binadamu, uharibifu wa kimwili na kiwewe cha pamoja kote Israel na eneo la Palestina linalokaliwa kwa mabavu," Guteers amemwambia rais wa Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Mataifa katika barua.
"Takriban watu 250 walitekwa nyara, wakiwemo watoto 34, zaidi ya 130 kati yao wakiwa bado mateka. Lazima waachiliwe mara moja na bila masharti. Habari za unyanyasaji wa kijinsia wakati wa mashambulizi ni ya kutisha."
Gutteres amesema "hakuna mahali salama huko Gaza."
"Tunakabiliwa na hatari kubwa ya kuanguka kwa mfumo wa kibinadamu. Hali inazidi kuzorota na kuwa janga lenye athari zisizoweza kutenguliwa kwa Wapalestina kwa ujumla na kwa amani na usalama katika eneo hilo," amesema.
Kifungu cha 99 cha UN kina umuhimu gani?
Mara ya kwanza UN ilitumia Kifungu cha 99 illkuwa tarehe 13 Julai 1960, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa wakati huo Dag Hammarskjöld aliomba mkutano wa dharura wa Baraza la Usalama chini ya Kifungu cha 99.
Hii ilikuwa kutokana na hali iliyokuwa imetokea katika Jamhuri ya Kidemocrasia ya Congo iliyokuwa imepata uhuru mwaka huo huo.
Ndani ya wiki moja baada ya kupata uhuru kutoka kwa Ubelgiji, Congo (ambayo baadae iliitwa Zaire na sasa inajulikana kama DRC) ilitumbukia katika mgogoro wa wenyewe kwa wenyewe ambao uligeuka kuwa mzozo wa kisiasa na kikatiba na ukadumu kwa takriban miaka mitano.
Katibu wa Umoja wa Mataifa aliomba kutumwa kwa dharura kwa msaada wa kijeshi nchini humo.
Mwaka wa 1961 rufaa hii ya Kifungu cha 99 kilitumika kwa ajili ya Tunisia.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa alisema ilikuwa kwa madhumuni ya kuzingatia malalamiko ya Tunisia dhidi ya Ufaransa "kwa vitendo vya uchokozi vinavyokiuka uhuru na usalama wa Tunisia na vitisho vya amani na usalama wa kimataifa."
Tunisia ililalamika kuwa kuwa tangu tarehe 19 Julai 1961 Ufaransa ilikuwa ikifanya uvamizi wa silaha, uliopangwa kimakusudi na ulioendelea dhidi ya Tunisia.
Ilisema ilikuwa imefanya kila juhudi kwa kutumia kidiplomasia njia ya kupata uhamishaji wa vikosi vya kigeni kutoka eneo lake lakini juhudi hizo hazikuzaa matunda yoyote.
Katibu mkuu alisema jitihada zaidi zilikuwa muhimu kwani wito wa usitishaji mapigano haukusababisha kusitishwa kwa unyanyasaji huo kwa kasi inayotakiwa.
Hata hivyo, kuna wale ambao wameikosoa Umoja wa Mataifa kwa kukosa kutumia kifungo hicho nchini Rwanda mwaka 1994, huku hali ya usalama ya Rwanda ikiporomoka kabla ya mauaji ya kimbari ambayo yalitokea licha ya tahadhari kutolewa awali.