Raia wa China waliohamishwa kutoka Sudan wakipeperusha bendera walipowasili katika kambi ya jeshi la wanamaji la Mfalme Faisal huko Jeddah. April 26, 2023.

China imetuma jeshi lake la wanamaji kuwaokoa raia kutoka Sudan iliyokumbwa na mzozo, wizara ya ulinzi mjini Beijing ilisema.

Jeshi la wanamaji lilitumwa Jumatano, msemaji wa wizara ya ulinzi ya China Tan Kefei alisema Alhamisi, "ili kulinda maisha na mali ya watu wa China nchini Sudan". Hakutaja idadi ya vyombo vilivyohusika.

China ilisema Jumatatu iliwahamisha kundi la awali la raia salama, ikikadiria takriban raia wake 1,500 walikuwa nchini Sudan.

Na Jumatano jioni Wu Xi, mkuu wa masuala ya kibalozi katika wizara ya mambo ya nje, aliambia shirika la utangazaji la CCTV zaidi ya raia 1,100 wa China - ikiwa ni pamoja na wakaazi wa Hong Kong - walikuwa wamehamishwa.

Raia 800 wa China watahamishwa kutoka Sudan kwa njia ya bahari kuanzia Aprili 25 hadi 27, msemaji wa wizara ya mambo ya nje Mao Ning alisema Jumatano.

Zaidi ya watu wengine 300 wamevuka hadi nchi zinazopakana na Sudan kwa ardhi, aliongeza.

China inasema kuwa ni mshirika mkubwa zaidi wa kibiashara wa Sudan, huku zaidi ya makampuni 130 yakiwekeza huko katikati ya mwaka 2022.

TRT World