Mapema wiki hii, Putin alionesha nia na utayari wake wa kuitembelea Uturuki./ Picha: AFP

Rais wa Urusi Vladimir Putin amepongeza nia ya kiongozi mwenzake wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan katika kukuza uhusiano kati ya nchi hizo mbili.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari siku ya Alhamisi katika mji mkuu wa Kazakhstan, Astana, Puntin aligusia kuwa vikwazo ya nchi za magharibi vilikuwa vinadhoofisha maendeleo ya ushirikiano wa kiuchumi kati ya Urusi na Uturuki.

"Kinachozuia (maendeleo ya mahusiano) kinajulikana. Kinachosaidia (mahusiano) kusonga mbele (ni) nia ya kisiasa ya Rais Erdogan," alisema Putin.

Katika kikao chake na Erdogan, pembezoni mwa Mkutano wa ushirikiano wa Shanghai siku ya Jumatano, Putin alisema: “Uhusiano kati ya Urusi na Uturuki unaendelea licha ya changamoto zilizopo duniani."

Uhusiano mzuri

Kwa upande wake, rais wa Uturuki alisema: "Njia ya nchi yetu ni imara na inaendelea kuimarika, na tunataka kuendeleza uhusiano wa joto kati ya Urusi na Uturuki."

Mapema wiki hii, akigusia uhusiano imara wa nchi yake, Putin alionesha nia yake ya kuitembelea tena Uturuki.

Viongozi hao walifanya mazungumzo ya simu ya mara kwa mara, wakijadiliana masuala ya nchi mbili na masuala ya kikanda.

TRT Afrika