Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu imetoa hati ya kukamatwa Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu na waziri wake wa zamani wa Ulinzi Yoav Gallant.
"Mahakama imetoa hati dhidi ya Benjamin Netanyahu na Yoav Gallant, kwa uhalifu dhidi ya ubinadamu na kusababisha vita kutoka Oktoba 8 2023 mpaka Mei 20, 2024, siku ambayo upande wa mashtaka ulituma hati hizo," taarifa imesema.
Kwa kufanya hivyo, mahakama ya ICC imepangua hoja ya Israeli iliyokuwa inadai kuwa mahamaka hiyo haina uwezo wa kusikiliza shauri hilo.
Katika madai hayo, mahakama hiyo ilisema kuwa inaamini kwamba "kila mmoja anawajibika kwa utekelezwaji wa uhalifu huo, hususani mauaji na mateso ya binadamu."
Hati hizo zimetolewa wakati mauaji ya kimbaro katika eneo la Gaza yameingia mwaka wa pili, yakiwa yameua zaidi ya Wapalestina 44,000, wengi wakiwa ni akina mama na watoto, na kujeruhi zaidi ya watu 103,000.
Mahakama hiyo pia imetoa hati ya kukamatwa kwa kiongozi mwandamizi wa Hamas Mohammed Diab Ibrahim Al-Masri, anayefahamika zaidi kama Deif.