Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF) limetangaza kuwa uamuzi wake uliokuwa ukisubiriwa kwa muda mrefu kuhusu wenyeji wa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2025 na 2027 utajulikana baadaye mwezi huu.
Shirikisho la CAF limetoa taarifa kuwa wenyeji hao watajulikana baada ya kikao cha kamati kuu ya CAF kufanyika mjini Cairo Septemba 27.
Hata hivyo uamuzi wa CAF ulitarajiwa kufanyika mapema mwaka huu baada ya CAF kutangaza kuwa walikuwa wakifungua tena zabuni kabla ya kuahirisha uamuzi huo mara kadhaa.
Wataalam huru wa ukaguzi waliteuliwa na CAF huku wakitembelea nchi zote zilizowasilisha zabuni, kwa minajili ya kuteuliwa kuwa mwenyeji wa mashindano hayo.
Kikosi hicho cha wataalam watatu kutoka kampuni ya PricewaterhouseCoopers (PwC) iliyojumuisha Adam Vojtekovszk, Omar El Ghiati, na Lakshmikanth Karunanithi, walikagua viwanja nchini Uganda, Kenya na Tanzania.
Shirikisho la kandanda la CAF limesema kuwa limepokea ombi kutoka Algeria, Morocco, Zambia, huku Benin na Nigeria, wakiwasilisha ombi la pamoja kuandaa kombe la Afcon 2025 huku Algeria, Botswana, Misri wakiwania kuandaa michuano ya 2027 dhidi ya ombi la pamoja kutoka Kenya, Tanzania na Uganda.