Mabingwa mara tatu wa Afcon, Super Eagles wa Nigeria ni mojawapo ya timu zilizofuzu kwa kombe hilo baada ya kuizamisha Sierra Leone 3-2. Osimhen alihamisha fomu yake iliyoisaidia Napoli kutwaa ubingwa wa Ligi kuu nchini Italia, kwa kutia kimiani magoli mawili kabla ya Kelechi Iheanacho kupachika bao la tatu na la ushindi.
Mabao ya Osimhen yalimwezesha kumpiku Sadio Mané kwenye orodha ya wafungaji bora kwenye mechi za kufuzu.
Vilevile, Cape Verde walitumia nafasi yao ya kuwa nyumbani kwa kuiadhibu Burkina Faso 3-1 katika mchuano uliogaragazwa Estádio Nacional de Cabo Verde.
Matokeo hayo yaliwashangaza Burkina Faso, waliofika nusu fainali katika makala yaliyopita ya Afcon 2021, nchini Cameroon.
Nchini Zambia, wenyeji Chipolopolo waliwapa Cote d'Ivoire kichapo kisichosahaulika cha 3-0 katika uga wa Levy Mwanawasa, mjini Ndola. Hata hivyo, licha ya kupoteza mechi, Cote d'Ivoire tayari walikuwa wamefuzu kwani ni waandalizi wa dimba la mataifa bora barani Afrika CAF TotalEnergies.
Kwingineko, licha ya Mchezaji wa zamani wa timu ya taifa ya Ufaransa, aliyebadili uraia kuichezea CAR, Geoffrey Kondogbia, kusawazisha goli la kwanza la Angola la Kialonda Gaspar, Winga wa Angola anayeichezea klabu ya Ankaragücü, nchini Uturuki, Felicio Milson, aliifungia Angola goli la pili na la ushindi la kunako dakika ya 86.
Aidha, watasalia kujilaumu baada ya kipa Dominique Junior Youfeigane kulishwa kadi nyekundu katika dakika ya 70.
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo DRC ilirejea na alama tatu muhimu kapuni kutoka Gabon baada ya kujiwekea ushindi wa 2-0 huko Franceville nayo Msumbiji ilizamisha matumaini ya Rwanda baada ya kuilaza 2-0.
Magoli ya Aaron Tshibola na Fiston Mayele yalitosha kuwapa chui wa DRC ushindi huo na kupiga jeki azma yao ya kutua Abidjan mapema mwaka ujao. Vijana wa Sébastien Desabre sasa wana alama 7 huku wakiwa wamesalia na mechi mbili.
Aidha, Mbweha wa jangwani; Algeria, waliwalemea wenyeji Uganda kupitia magoli ya Mohamed El Amine Amoura. El Amine aliihakikishia timu yake nafasi kwenye ngarambe za Afcon 2023, baada ya kufunga magoli mawili na kufikisha pointi za Algeria hadi 12.
Mjini Dar es Salaam, wenyeji Taifa Stars wa Tanzania, walirejesha tabasamu kwenye nyuso za mashabiki waliofurika katika uwanja wa Kitaifa baada ya kuifunga Niger 1-0.
Goli la Simon Msuva lilitosha kuipa Tanzania alama tatu muhimu na kuzidisha matumaini yake ya kuingia Afcon ikiwa katika nafasi ya pili kwenye kundi F ikiwa na alama 7.
Mechi tatu zilizosalia katika raundi hii ya michuano ya kufuzu, zitachezwa Jumanne, tarehe 20 mwezi huu huku Ethiopia ikiipokea Malawi kwenye kipute cha kundi D. Aidha, Namibia itafunga safari hadi Bujumbura kumenyana na wenyeji Burundi katika mechi ya kundi C, huku Sudan ikiilaki Mauritania katika mechi iliyosalia ya kundi I.
Sudan itakuwa inalenga kulipiza kisasi dhidi ya Mauritania baada ya kulazwa 3-0 mjini Nouakchott mwaka uliopita.