Nyota chipukizi wa Ac Milan ya Italia Francesco Camarda ameweka historia Jumamosi baada ya kuwa mchezaji mdogo kabisa kuwahi kushiriki mechini Serie A kwenye pambano ambalo Milan ilijipa ushindi wa 1-0 dhidi ya Fiorentina, siku ya Jumamosi.
Camarda amefuta rekodi ya awali iliyowekwa na beki wa Bologna Wisdom Amey, ambaye alishiriki mechi yake ya kwanza ya Serie A akiwa na umri wa miaka 15, miezi tisa na siku moja, mnamo Mei 2022.
Camarda aliingia kwenye vitabu vya historia baada ya kuingia uwanjani kuchukua nafasi ya Luka Jovic kunako dakika ya 83 ugani San Siro akiwa na umri wa miaka 15, miezi minane na siku 15.
Camarda aliitwa kikosi kikuu kutoka upande wa vijana wa Milan kukamilisha safu ya Milan kutokana na kutokuwepo kwa wachezaji wakiwemo Olivier Giroud, Rafael Leao na Noah Okafor.
"Ana talanta nyingi na akili, anajua kwamba anahitaji kufanya kazi kwa bidii kuliko kila mtu mwingine," alisema nahodha wa klabu ya Milan Davide Calabria baada ya mchuano huo.
Milan ni inashikilia nafasi ya tatu kwenye ligi kuu ya Serie A, ikiwa pointi tano nyuma ya viongozi wa ligi hiyo Inter Milan ambayo itakabiliana na Juventus siku ya jumapili.