"Manchester United inafuatilia madai yaliyotolewa dhidi ya Antony/ Picha : Reuters

Winga wa klabu ya Manchester United Antony hatarejea klabuni mara moja huku akishughulikia tuhuma za unyanyasaji wa kingoni zinazomkabili.

"Manchester United inafuatilia madai yaliyotolewa dhidi ya Antony," klabu hiyo ilisema katika taarifa fupi.

Antony aliondolewa kwenye kikosi cha Brazil kwa mechi mbili za kufuzu Kombe la Dunia huku kukiwa na uchunguzi wa polisi kuhusu madai yaliyotolewa na mpenzi wake wa zamani Gabriela Cavallin ya unyanyasaji wa kingono. Antony amekana kosa lolote.

"Wachezaji ambao hawajashiriki mechi za kimataifa wanatarajiwa kurejea mazoezini Jumatatu. Hata hivyo, tumekubaliana na Antony kwamba atachelewesha kurejea kwake hadi itakapotangazwa tena ili kushughulikia tuhuma hizo,'' taarifa hiyo ilisema.

Antony Matheus dos Santos,( 23) anayejulikana kwa urahisi kama Antony, ni mchezaji wa soka wa Brazil ambaye anacheza kama winga wa klabu ya Ligi ya England Manchester United na timu ya taifa ya Brazil.

Alijiunga na Man U mwaka 2022, na kabla y ahapo alichezea klabu ya Ajax kwa miaka miwili kuanzia 2020, alikoanzia kuchezea klabu za kimataifa.

"Nimekubaliana na Manchester United kuchukua muda wa kutokuwepo wakati nikishughulikia tuhuma zilizotolewa dhidi yangu," mchezaji huyo aliandika kwenye chapisho kwenye Instagram. "Huu ulikuwa uamuzi wa pande zote ili kuepuka usumbufu kwa wachezaji wenzangu na mabishano yasiyo ya lazima kwa klabu.

TRT Afrika na mashirika ya habari