Mshambulizi wa Norway Erling Haaland alifunga bao lake la 100 kwa Manchester City mnamo Septemba 22, 2024. / Picha: Reuters

Arsenal ikiwa na wachezaji kumi ilitoka sare ya 2-2 dhidi ya Manchester City katika mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kwenye Uwanja wa Etihad Jumapili.

Manchester City walikuwa wa kwanza kupata bao kupitia kwa Erling Haaland katika dakika ya 9. Bao hilo lilimfanya mshambuliaji huyo wa Norway kufikisha mabao 100 akiwa na City katika mechi 105 alizocheza.

Arsenal walisawazisha katika dakika ya 22 kupitia kwa mchezaji wa beki Riccardo Calafiori.

Arsenal walijiweka mbele katika dakika za mwisho za kipindi cha kwanza kupitia kwa Gabriel mpira wa kichwa, kutoka kwa kona ya Bukayo Saka.

Kadi nyekundu ya Arsenal

Katika dakika za mwisho za muda ulioongezwa kipindi cha kwanza, Leandro Trossard alionyeshwa kadi ya pili ya njano na mwamuzi Michael Oliver, hivyo kuwaacha Arsenal wakiwa na wachezaji kumi uwanjani.

Jaribio la Gunners kulinda bao lao lilikaribia kufanikiwa, hadi dakika za lala salama katika kipindi cha pili, wakati John Stones wa Manchester City alipopiga shuti kwenye wavu wa Arsenal na kusawazisha, na kuvunja mioyo ya wachezaji wa Arsenal.

Kufuatia matokeo hayo ya Jumapili, City wanashikilia nafasi yao ya kwanza kwenye jedwali la EPL wakiwa na pointi 13 baada ya michezo mitano, mbele ya Liverpool (pointi 12), Aston Villa (pointi 12), Arsenal (pointi 11), Chelsea (pointi 10) na Newcastle (pointi10).

Vijana wa Pep Guardiola watacheza ugenini Septemba 28 dhidi ya Newcastle United, huku vijana wa Mikel Arteta wakiwapokea wageni Leicester City siku hiyo hiyo.

TRT Afrika