Taifa la Somalia limeandaa kongamano lililojumuisha raia wake waliorejea nyumbani nchini humo baada ya kuishi ng'ambo kwa muda mrefu.
Kongamano hilo, ambalo ni la pili kufanyika tangu kumalizika kwa vita vya ndani nchini humo, liliandaliwa na Wizara ya masuala ya nchi za kigeni mjini Mogadishu na kuwaleta pamoja wasomi, wawekezaji, wanafunzi, viongozi wa kisiasa na vijana waliohitimu masomo ya kiwango cha juu nje ya nchi yao.
“Jamii za Wasomali wanaoishi nje ya nchi zina jukumu muhimu katika maisha ya Wasomali kupitia uhamishaji fedha, usaidizi wa kibinadamu na ushiriki katika juhudi za ujenzi upya wa taifa letu” Alisema Waziri Abshir Omar Jama, baada ya kulifungua kongamano hilo.
Hata hivyo, wengi wao hudumisha uhusiano wao wa karibu na nchi yao na huchukua jukumu muhimu katika ujenzi wake kupitia uhamishaji fedha, uwekezaji na uhamisho wa ujuzi na kupunguza changamato za chakula, afya, elimu, na mahitaji mengine.
Raia wa Somalia wanaoishi nje ya nchi hiyo, waliweza kufanikisha mabilioni ya dola kupitia njia ya kutuma pesa na kuwa na mchango mkubwa kwa ukuaji wa uchumi wa taifa hilo.
Miongoni mwa masuala yaliyojadiliwa ni uchumi wa nchi, ujenzi wa serikali, na kusaka mbinu za kuboresha mahitaji ya raia wa nchi walioko ughaibuni.
Wengine walioshiriki ni Mawaziri wa Serikali ya Somalia, wabunge, maseneta, wawakilishi wa asasi za kiraia, na wanachama wa muungano wa Wasomali walioko ughaibuni.