Mwanaisha Chidzuga naibu msemaji wa Serikali ya Kenya. Picha: Mwanaisha Chidzuga

Mwanahabari maarufu wa kike nchini Kenya ambaye amejizolea sifa kwa usomaji habari za Kiswahili katika runinga Mwanaisha Chidzuga, ametangazwa kuwa naibu msemaji wa serikali ya Kenya huku akiwa mwandishi wa pili wa kike nchini humo kuteuliwa. Kanze Dena alikuwa ni mwanamke wa kwanza mwandishi kuwa msemaji wa serikali iliyotoka madarakani ya Uhuru Kenyatta.

Baada ya tangazo la uteuzi wake, Chidzuga aliandika ujumbe wa shukrani kwa rais William Ruto, huku akiahidi kuutumia wadhifa huo vyema.

"Kwanza kabisa, ningependa kutoa shukrani zangu za dhati kwa rais wetu William Samoei Ruto, CGH, na chama tawala kwa kuweka imani yao kwangu. Uteuzi huu unawakilisha hatua muhimu, sio tu katika taaluma yangu, lakini pia katika muktadha mpana wa usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake," Chidzuga aliandika.

Mwanaisha Chidzuga aliwania kiti cha ubunge cha eneo bunge la Matuga kupitia chama cha rais William Ruto cha (UDA). Picha: William Ruto

"Kama mteule wa jukumu la naibu Msemaji wa Serikali, ninakuja mbele yenu leo kwa moyo uliojaa shukrani na hisia ya kina ya heshima. Ni heshima kukabidhiwa jukumu hili, na ninanyenyekea kwa fursa ya kuitumikia nchi yangu kwa njia hii."

Chidzuga, ambaye amefanya kazi katika mashirika ya kitaifa ya habari nchini Kenya kama vile KBC, K24 na TV-47, alifanya jaribio lake la kwanza la kisiasa alipogombea katika uchaguzi uliopita nchini Kenya, alipojaribu kufuata nyayo za marehemu mama yake Zainab Chidzuga, ambaye aliwahi kuwa mwakilishi wa wanawake wa Kwale kati ya mwaka 2017-2017.

Tangazo la uteuzi wa Mwanaisha Chidzuga. Picha: Hussein Mohamed, Msemaji wa Ikulu Kenya.

"Ninaahidi kutekeleza majukumu yangu kwa kujitolea kwa utaalum mkubwa, wakati pia nikijitahidi kuwa mfano wa kuigwa kwa wanawake wengine wachanga wanaotamani kuvunja vizuizi na kufikia ndoto zao. Mwanaisha Chidzuga.

Mtangazaji huyo wa zamani wa televisheni aliwania kiti cha ubunge cha eneo bunge la Matuga kupitia chama cha rais William Ruto cha (UDA) lakini alipoteza kiti hicho kwenye kinyang'anyiro kilichowashirikisha washindani wengi ikiwa ni pamoja na kaka yake mkubwa, Hassan Chidzuga.

TRT Afrika