Pan-Africanism iliibuka mwishoni mwa karne ya 19 na mwanzoni mwa karne ya 20. Picha: Picha za Getty

Na

Dwomoh-Doyen Benjamin

Katika kuzungumzia tofauti baina ya binadamu, dhana ya utambulisho mara nyingi hufunika mipaka ya kijiografia, tamaduni asilia, na urithi wa kihistoria.

Kwa kuzingatia hayo, vuguvugu la Muungano wa Afrika linasimama kama kanuni inayoelekeza, sio tu kwa maneno matupu bali kama utambulisho wa ndani unaoakisi asili, mapambano, na matumaini yanayofanana ya watu mbalimbali lakini waliounganishwa katika mabara tofauti.

Katika msingi wake, harakati za Muungano wa Afrika zinavuka mipaka ya kijiografia ya bara la hili, ukikumbatia watu wote wenye asili ya Kiafrika, haijalishi wamekita mizizi yao barani humu au wametawanyika ulimwenguni kwa sababu za uhamiaji na dhuluma za kihistoria.

Dhana hii inaibua utambulisho wa kweli, badala ya kuonekana kama dhana ya kufikirika tu—ambayo inawaunganisha watu chini ya bendera ya urithi mmoja.

Muktadha wa Kihistoria:

Harakati hizi za kuunganisha Afrika zilizoibuka mwishoni mwa karne ya 19 na mwanzoni mwa karne ya 20, zinawakilisha utambulisho wenye nguvu uliojengeka katika mapambano, ndoto, na matumaini yanayofanana ya watu wenye asili ya Kiafrika kote duniani. Ili kuelewa umuhimu wa harakati hizi, lazima tuchimbe undani wake kihistoria.

Pan-Africanism inaashiria ujumuishi. Picha: AFP

Zikiwa zimezaliwa kutokana na historia ya ukoloni, utumwa, na ubaguzi wa rangi, harakati za Muungano wa Afrika zilijitokeza kama mwitikio wa mapambano dhidi ya madhila yanayowakabili watu wenye asili ya Kiafrika ulimwenguni kote.

Jitihada hizi ziligeuka jukwaa kwa wale waliokumbwa na athari hizo na kuwasukuma kuungana ili kushughulikia masuala ya mfumo yanayosumbua jamii zao. Kipande cha neno "Pan" katika Pan-Africanism kinawakilisha wigo mpana unaogusa ulimwengu wote.

Kinatambulisha kumbatio la karibu la asili ya Kiafrika—kupita vikwazo vya kikabila, mipaka ya kitaifa, na matabaka ya kijamii.

Muungano huu unawahimiza watu kujitambua wenyewe sio kwa kufuata misingi ya kabila au taifa bali kama sehemu ya familia kubwa, iliyounganishwa na Uafrika wao.

Diaspora na Urithi Shirikishi

Ni muhimu kutambua muktadha wa kihistoria wa Waafrika waishio nje ya bara hili (diaspora) na wale wa visiwa vya Caribean, ambapo idadi isiyohesabika ya watu walihamishwa kwa nguvu kutoka kwa familia zao za Kiafrika na kuuzwa utumwani. Muungano huu unawaalika wale katika diaspora kutafuta asili zao za Kiafrika na kurejesha urithi wao.

Kwa kutambua kwamba wote wana damu yenye asili ya Afrika, watu wa diaspora wanaweza kuimarisha uhusiano wao kupitia harakati hizi, wakielewa kuwa wao ni sehemu muhimu ya familia kubwa ya Kiafrika.

Kwame Nkrumah wa Ghana na Jamal Abdul Nasser wa Misri

Kwame Nkrumah wa Ghana na Jamal Abdul Nasser wa Misri

Fikiria ulimwengu ambapo mtu kutoka Kisiwa cha Shelisheli, Burkina Faso, Nigeria, Kenya, Afrika Kusini, Misri, Ghana, Caribean, au Mmarekani mweusi kutoka Marekani anajitambulisha kama Mwafrika bila maswali lukuki kuhusu asili yake, kabila lake au anatoka upande gani wa Afrika.

Mazingira yaliyopo sasa mara nyingi yanapelekea mfululizo wa maswali chokonozi —yakiakisi hulka ya binadamu ya kutenganisha na kugawanya.

Hivyo, kwa kufuata mtazamo wa vuguvugu hili, watu wanaweza kupata hisia na kujiona wanahusika na kujitambua wenyewe kama sehemu ya familia kubwa ya Kiafrika inayojumuisha tamaduni, historia, na mchango mbalimbali.

Kama vile mtu anavyoweza kutambulika kutokana na nchi au kabila, wanaweza pia kutambua Afrika kama mahali pao pa asili.

Nguvu ya harakati hizi zinategemea uwezo wake wa kuunganisha kundi kubwa. Fikiria idadi ya zaidi ya watu bilioni moja barani Afrika pekee, pamoja na mamilioni wanaoishi ughaibuni, kuanzia Caribean hadi Marekani na Ulaya.

Kukubali utambulisho unaotuunganisha utawafanya kundi hili la watu kuwa familia kubwa zaidi duniani—familia yenye uwezo wa kukuza umoja, uthabiti, na maendeleo.

Mshikamano wa Kiuchumi

Muungano huu wa Watu wenye asili ya Afrika unakuja na utambuzi wa umuhimu wa mshikamano wa kiuchumi. Unahimiza ukuzaji wa ushirikiano wa kiuchumi, biashara, na uwekezaji ndani ya bara la Afrika, ukirahisisha ukuaji na maendeleo ya mataifa na watu wa Kiafrika.

Kwa kuunganisha nguvu za kiuchumi, watetezi wa vuguvugu hili wanatafuta kushinda ukoloni na upotezaji wa rasilimali ambao umekwamisha maendeleo ya Afrika.

Hata hivyo, njia ya umoja huu sio juhudi binafsi pekee; inahitaji jitihada za pamoja kutoka kwa mashirika kama Umoja wa Afrika na vyombo vingine vya kikanda.

Elimu inasimama kama nyenzo imara katika harakati hizi—chombo cha kuwaelimisha watu kuhusu kiini cha Umoja huu, si kama wazo la kifalsafa bali kama sehemu ya ndani ya utambulisho wao na asili yao. Ni wito kwa ndugu na dada wa Kiafrika kuwa walinzi wa wenzao.

DR Congo, one of the richest countries in term of minerals, aims to save informal cobalt miners from swindlers. Photo: AFP

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, mojawapo ya nchi tajiri zaidi kwa rasilimali za madini, inalenga kuokoa wachimbaji wa kobalti wasio rasmi wanaohadaiwa.

Muungano wa Afrika, kwa asili yake, sio dhana inayojadiliwa kwenye mihadha wala mikutano au mazungumzo ya kitaaluma; ni wito wa hatua, mwito wa kutambua kwa dhati asili ya pamoja na hatima.

Ni mbinu ya kuepuka mtazamo wa kutugawanya uliyoingizwa kwenye mifumo ya kijamii na kukomaza umoja unaovuka vizazi na mabara.

Inawaalika kila mtu mwenye asili ya Kiafrika kutambua asili zao, kuzisheherekea kama nyuzi zilizounganishwa katika kitambaa chenye rangi nyingi cha urithi wa Kiafrika— urithi unaounganisha badala ya kutenganisha.

Watu wote wa Kiafrika bila kujali kabila au asili ya kitaifa wanapaswa kufundishwa kuona fahari juu ya utambulisho wa kama Waafrika.

Harakati na taasisi ya Umoja wa Afrika (AU)

Vuguvugu hili linapaswa kutumika kama msingi wa Umoja wa Afrika, taasisi iliyodhamiria kukuza umoja na ushirikiano katika bara hili.

Kupitia vuguvugu hili, Umoja wa Afrika unaweza kuweka maslahi ya Waafrika wote mbele na kutafuta Afrika iliyounganika inayovuka mipaka ya kitaifa, mgawanyiko wa kikabila, na urithi wa ukoloni.

Umoja huu ungeongeza sauti na juhudi za pamoja za Waafrika, kuwawezesha kukabiliana na changamoto kubwa, kufikia ustawi wa kiuchumi, na kudumisha kanuni za haki na usawa.

Harakati hii inasisitiza jukumu muhimu la utamaduni na utambulisho

Kwa kuikumbatia falsafa hii kama utambulisho wa kweli, tunajenga mustakabali ambapo watu wanajitambulisha kwa kujivunia kama Waafrika, wakisimama imara katika urithi wao na kujenga madaraja yanayowaunganisha kote duniani.

Hii sio ndoto; ni ukweli unaosubiriwa kwa hamu na kila mmoja wetu—ukweli ambapo umoja unashinda mgawanyiko, na familia kubwa zaidi duniani inasimama kwa umoja.

TRT Afrika