Kupitia taarifa rasmi iliyotolewa na Ikulu, rais Samia ametenganisha Wizara ya awali ya Fedha na Mipango iliyokuwa ikiogonzwa na Waziri Dkt Mwigulu Nchemba, na badala yake kubuni Wizara ya Fedha na Wizara ya Mipango huku itakayofahamika kuwa Wizara ya Nchi katika Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji.
Kufuatia kutungwa kwa Sheria ya Mipango ya Taifa ya Mwaka 2023 pamoja na uamuzi wa kuhamishia masuala ya uwekezaji ya Ofisi ya Rais, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amefanya mabadiliko madogo ya Miundo ya Wizara na kufanya uteuzi wa viongozi. Ikulu iliandika.
Aidha, Profesa Kitila Mkumbo ambaye pia ni Mbunge wa Ubungo, na Mhadhiri maarufu wa muda mrefu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ameteuliwa kuiongoza wizara hiyo.
Profesa Kitila pia anarejea kwenye jopo la mawaziri baada ya kulitumikia taifa hilo hapo awali kama Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uwekezaji), Wizara ya Viwanda na Biashara na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji.
Kulingana na Taarifa ya ikulu, Rais Samia amebuni Wizara ya Viwanda na Biashara itakayosimamiwa na Dkt. Ashatu Kijaji ambaye kabla ya uteuzi huo, alishikilia Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara, ambayo sasa imefanyiwa mabadiliko.
Taarifa hiyo pia imeeleza kuwa Rais ameunda Wizara mpya ya Viwanda na Biashara na amemteua aliyekuwa Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Dk Ashatu Kijaji kuwa Waziri wa wizara hiyo.
“Amemteua Laurence Mafuru kuwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango ya Taifa. Kabla ya uteuzi huo, Mafuru alikuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha na Mipango (usimamizi wa uchumi)."
“Amemteua pia Elijah Mwandumbya kuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha (usimamizi wa uchumi), kabla ya uteuzi huo Mwandumbya alikuwa Kamishna, Idara ya Uchambuzi wa Sera, Wizara ya Fedha na Mipango."
Uteuzi na Mabadiliko yaliyofanyika, yametimia miezi mitano tu huku yakiambatana na nia ya Rais Samia baada ya kueleza mipango yake ya kuunda Tume ya Mipango.