Mheshimiwa Paul Kagame, Rais wa Rwanda anafanya ziara ya Kikazi nchini Tanzania kuanzia tarehe 27 hadi 28 April, 2023.
Kagame na Ujumbe wake waliwasili kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere hii leo ambapo baadae walifanya mazungumzo na Rais wa Jamuhuri ya muungano wa Tanzania mama Samia Suluhu Hasan.
Lakini je ni maeneo gani yanayoiunganisha Rwanda na Tanzania katika mahusiano yao ya kidiplomasia?
Biashara: Kiwango cha biashara kati ya Tanzania na Rwanda kimekuwa kikiongezeka mwaka hadi mwaka huku Tanzania ikiuza zaidi bidhaa za chakula na nafaka, hususan mchele na mahindi, bidhaa za viwandani kama madawa, mbolea, mafuta na mipira.
Bandari: Mamlaka ya Bandari Tanzania imefungua Ofisi nchini Rwanda kwa ajili ya kuimarisha huduma kwa wateja. TPA inahudumia zaidi ya asilimia 83 ya shehena za mizigo ya Rwanda. Huku serikali ya Rwanda ikikusudia kutumia zaidi Bandari ya Tanga kama njia ya kusafirisha shehena ya mizigo yake
Umeme: Tanzania, Rwanda na Burundi zinashirikiana kutekeleza mradi wa kuzalisha umeme wa maji wa Rusumo unaotarajiwa kuzalisha Megawatt 80. Kwa mujibu wa taarifa ya serikali mradi huo umefikia asilimia 98.5 na unatarajia kukamilika mwezi Agosti 2023
Reli: Mwaka 2005, Tanzania, Rwanda na Burundi, kwa pamoja zilikubaliana kujenga reli mpya ya kisasa kutoka Isaka hadi Kigali itakayo ungana na Burundi kuanzia Keza hadi Musongati kupitia Gitega.
Tanzania na Rwanda zimekuwa na uhusiano mzuri wa kidiplomasia uliodumu kwa muda mrefu ambapo nchi hizi mbili zimekuwa zikishirikiana kwenye sekta mbalimbali za kimkakati ikiwemo biashara na uwekezaji, nishati, uchukuzi, elimu na utamaduni.
Kufanyika kwa ziara hii ni ishara nzuri ya kuendelea kumarika kwa uhusiano wa kidugu baina ya mataifa haya kwa maslahi mapana ya pande mbili.