Viongozi wa kijeshi wa Niger wamekataa kuachilia familia ya rais aliyezuiliwa katika mapendekezo ya ishara ya nia njema, kwa mujibu wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken.
Hofu imekuwa ikiongezeka kwa afya ya rais Mohamed Bazoum pamoja na mkewe na mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka 20 tangu jeshi lilipochukua mamlaka na kuwachukua mateka Julai 26.
Katika mazungumzo ya simu na rais wa zamani wa Niger Mahamadou Issoufou, Blinken "alionesha wasiwasi wake mkubwa kutokana na kuendelea kuwekwa kizuizini kinyume cha sheria chini ya hali mbaya ya Rais Bazoum na familia yake."
Blinken alieleza kuwa amesikitishwa sana na kukataa kwa wale walionyakua mamlaka nchini Niger kuwaachilia familia ya Bazoum kama ishara ya nia njema," taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ilisema Ijumaa.
Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell alisema kuwa Bazoum na familia yake wamenyimwa chakula, umeme na huduma za matibabu kwa siku kadhaa.
Mkuu wa haki za Umoja wa Mataifa, Volker Turk, alisema hali ya kizuizini ya Bazoum "inaweza kufikia unyanyasaji wa kinyama na udhalilishaji, unaokiuka sheria za kimataifa za haki za binadamu."