Kulingana na Shirika la Afya Duniani, WHO, asilimia 51 tu ya wanawake wajawazito hufanya ziara mara nne au zaidi za uchunguzi kabla ya kujifungua. WHO inapendekeza angalau ziara nane wakati wa ujauzito.
Ripoti moja ya Medical Xpress ilionesha Jumanne nchini Tanzania kuwa utafiti ulilenga athari za programu hiyo kwenye matokeo ya kujifunza ya wakunga na uandaaji wa kujifungua kwa wanawake wajawazito nchini Tanzania.
Kazi ya timu hiyo imechapishwa katika jarida la PLOS ONE tarehe 31 Machi 2023.
Timu ya watafiti ilikuwa pamoja na watanzania Beatrice Mwilike na Dorkasi Mwakawanga kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili, MUHAS, Tanzania.
Yoko Shimpuku, profesa katika Shule ya Uzamili ya Sayansi za Tiba na Afya katika Chuo Kikuu cha Hiroshima, alieleza kuwa programu ya simu ya mkononi kwa wakunga ilionyesha maboresho makubwa katika matokeo yao ya kujifunza, na hivyo kusababisha maandalizi bora ya kujifungua kwa wanawake wajawazito nchini Tanzania.
"Utafiti huu unasisitiza uwezo wa kutumia teknolojia kuimarisha elimu ya wakunga, na hatimaye kuchangia afya ya mama na kupunguza viwango vya vifo vya mama na mtoto," Shimpuku alinukuliwa akisema.
Utafiti huo uliwahusisha wakunga 23 ambao walishiriki katika majaribio na kutoa data za matokeo ya kujifunza. Matokeo yao yalionyesha kuwa asilimia 87.5 ya wakunga waliendelea kusoma na kutumia programu hiyo miezi miwili baada ya hapo.
Wanawake wajawazito 207 walishiriki katika utafiti huo. Kikundi kilichopata msaada wa programu kilikuwa na alama za maarifa za juu zaidi ikilinganishwa na wanawake katika kikundi ambapo programu haikutumika.
Alama hizo za utafiti pia zilionesha kuwa wanawake wanapenda zaidi kujifungua katika kituo cha afya badala ya nyumbani.
Shimpuku aliambia Medical Xpress kuwa lengo kuu ni kuendeleza programu nyingine zinazolenga wanawake wajawazito na familia zao, huku wakikusanya ushahidi imara juu ya athari na ufanisi wa muda mrefu wa programu hiyo kupitia utafiti zaidi.
"Hii inalenga kuimarisha uelewa na ufahamu wa jumla wa huduma kuanzia ujauzito hadi baada ya kujifungua, na hatimaye kuboresha afya ya mama," alisema Shimpuku.
Kutokana na kufanya tafiti za awali, timu ya watafiti ilijua kuwa kuna matumizi makubwa ya simu za kisasa nchini Tanzania, hasa miongoni mwa vijana.