Jeshi la Niger limekuwa likipambana na ongezeko la ghasia zinazotekelezwa na wanamgambo. /Picha: Reuters

Maafisa watatu na askari aliyekuwa akiwasindikiza waliuawa wiki hii, kusini magharibi mwa Niger na watu wenye silaha waliovuka mpaka kutoka Nigeria, mamlaka ilisema Jumapili.

"Siku ya Jumatano, watu wenye silaha kutoka Nigeria walishambulia gari na kuua watu wanne," jeshi lilisema, bila kuwataja wahasiriwa, shirika la habari la AFP linaripoti.

Ripoti ilisema washambuliaji kisha "wakarejea Nigeria."

Wenyeji walisema wanne hao walikuwa wakizuru Diffa, eneo ambalo limeshuhudia mfululizo wa mashambulizi mabaya tangu 2015 na wapiganaji wa Boko Haram.

Makazi ya vikundi vyenye silaha

Eneo la Diffa liko kwenye mwambao wa Ziwa Chad, ambalo linapakana na Cameroon, Chad, Niger na Nigeria. Visiwa vyake vyenye kinamasi vimekuwa maficho ya makundi yenye silaha.

Mto Komadougou Yobe, ambao ni mpaka kati ya Niger na Nigeria, hapo awali ulisaidia kulinda Diffa kutokana na mashambulizi ya mara kwa mara.

Lakini kiwango cha maji kimeshuka, na kusababisha kupatikana kwa "vivukio vingi kutoka Nigeria," ambayo iliwezesha wapiganaji wa wanamgambo kushambulia wasafiri kwenye barabara kuu, na hapo ndio shambulio la wiki hii lilitokea, jeshi lilisema.

Tangu kutokea kwa tukio hilo, mamlaka ya mkoa imeweka marufuku ya muda usiojulikana kwa magari "hasa ya 4x4" kusafiri bila kusindikizwa na jeshi barabarani, kwa umbali wa kilomita 70 (maili 40) kutoka mji wa Diffa hadi mji wa Maine Sorao.

Kupambana na ugaidi

Afisa wa zamani wa eneo hilo aliiambia AFP kwamba waviziaji "hulenga zaidi magari ya kifahari, ambayo wanayauza tena nchini Nigeria."

Katika eneo la magharibi la Tillaberi, karibu na mpaka wa Burkina Faso na Mali, wanajeshi wa Niger wanapambana na makundi mengine yenye uhusiano na Al-Qaeda.

Siku ya Jumamosi, mamia ya watu walifanya maandamano mjini Tillaberi, wakitoa wito kwa jeshi lilioko madarakani nchini Niger kuanzisha "vitengo vya uingiliaji wa haraka" na "kambi ya anga", na kuajiri "wajitolea" wa kiraia kusaidia mashambulizi makali dhidi ya wakazi wa eneo hilo.

Kikosi cha kijeshi, ambacho kilichukua mamlaka katika mapinduzi ya Julai 2023, kililalamika kwamba aliyekuwa rais Mohamed Bazoum hakufanya vya kutosha kukomesha mashambulizi.

TRT Afrika na mashirika ya habari