Kikosi cha kijeshi cha Niger siku ya Alhamisi kilisema kuwa kimebatilisha mikataba mbalimbali ya ushirikiano wa kijeshi na Ufaransa baada ya kuondolewa madarakani kwa Rais Mohamed Bazoum katika mapinduzi ya wiki iliyopita.
Ufaransa ina wanajeshi kati ya 1,000 na 1,500 nchini Niger, wanaosaidia kupambana na uasi wa makundi yenye mafungamano na al Qaeda na kile kinachojiita Dola la Kiislamu ambalo limeenea katika eneo la Sahel.
Ushirikiano wote wa kijeshi na itifaki na Ufaransa ''umesitishwa'', lilisema junta. Hili linaweza kuwa tatizo kwa Ufaransa kwani uhusiano wake na Mali na Burkina Faso tayari umedorora kufuatia mapinduzi ya kijeshi katika nchi hizo mbili.
Niger imekuwa ikipokea wanajeshi wa Ufaransa waliokuwa wamehama kutoka nchi jirani ya Mali. Kusitishwa kwa ushirikiano wa kijeshi kunaweza kuwaacha wanajeshi katika hali tete.
Wanajeshi hao pia wamewaita mabalozi wa nchi hiyo kutoka Ufaransa, Nigeria, Togo na Marekani.
Amadou Abdramane, msemaji wa Baraza la Kitaifa la Kulinda Nchi, alitangaza hatua hizo kwenye runinga ya serikali Alhamisi usiku.
Matukio ya kutiliwa shaka
Jeshi limetishia kushambulia nchi mwanachama wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi ECOWAS iwapo jumuiya hiyo ya Afrika Magharibi itaingilia kijeshi nchini humo.
"Uchokozi wowote au jaribio la uchokozi dhidi ya Jimbo la Niger utaona jibu la mara moja na la ghafla kutoka kwa Vikosi vya Ulinzi na Usalama vya Niger kwa mmoja wa wanachama (wa kambi hiyo)," alisema.
Hii haitawaathiri nchi waliona uhusiano wa karibu aliongeza, akigusia Guinea, Mali na Burkina Faso.
Kundi la kanda ya Afrika Magharibi ECOWAS lilikuwa limetishia kutumia nguvu kubadili mapinduzi ya Niger na kumrejesha Rais aliyeondolewa madarakani Mohamed Bazoum. Lakini umoja huo pia umetuma wajumbe kwenda Niamey kwa mazungumzo na viongozi wa mapinduzi.
Akitoa wito kwa jamii kuwa makini kuhusu majeshi na mawakala wa nchi za kigeni, Abdramane aliwataka watu wa Niger kuwafahamisha maafisa kuhusu matukio yoyote yanayotiliwa shaka.