Wakati wa mkutano na viongozi wa Kiislamu wa Nigeria, Jenerali Tchiani alisema yuko tayari kufanya mazungumzo na ECOWAS. Picha: Reuters

Utawala wa kijeshi wa Niger unasema uko tayari kufanya mazungumzo na jumuiya ya kanda ya Afrika Magharibi ECOWAS. Hii ni mara ya kwanza kwa viongozi wa mapinduzi kuashiria mlango wazi wa mazungumzo na chombo cha kikanda.

Umoja wa Afrika Magharibi ulikuwa umeiwekea Niger vikwazo na kutishia kutumia nguvu kubadili mapinduzi hayo. Jaribio la wiki iliyopita la kutuma timu ya pamoja ya wawakilishi wa ECOWAS, Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika mjini Niamey kwa mazungumzo lilikataliwa na viongozi wa mapinduzi hayo.

Hata hivyo, kufuatia ziara ya ujumbe wa wanazuoni wa Kiislamu wenye ushawishi kutoka nchi jirani ya Nigeria siku ya Jumamosi, junta ilisema kuwa sasa iko tayari kwa mazungumzo na jumuiya hiyo ya Afrika Magharibi.

Viongozi hao wa Kiislamu walifanya mazungumzo na kiongozi wa kijeshi Jenerali Abdourahmane Tchiani. Waziri Mkuu wa Niger aliyeteuliwa na junta, Ali Mahamane Lamine Zeine, aliwaambia waandishi wa habari mjini Niamey kwamba Jenerali Tchiani ametoa mwanga wa kijani kwa mazungumzo na ECOWAS.

Mazungumzo siku chache zijazo

Alipoulizwa kama junta iko tayari kufanya mazungumzo na ECOWAS, Waziri Mkuu alijibu: ‘’Ndiyo, kwa hakika. Ndivyo alivyowaambia kiongozi wa nchi yetu, hakusema kuwa hayuko tayari kufanya mazungumzo.’’

Waziri Mkuu alikuwa na matumaini kwamba mazungumzo na ECOWAS yangefanyika katika siku chache zijazo.

‘’Tumekubali na kiongozi wa nchi yetu ametoa mwanga kwa ajili ya mazungumzo. Sasa watarudi na kumjulisha Rais wa Nigeria kile walichosikia kutoka kwetu.... tunatumai siku zijazo, wao (ECOWAS) watakuja hapa kukutana nasi ili kujadili jinsi vikwazo vilivyowekwa dhidi yetu vitaondolewa,'' alisema.

Viongozi wa Kiislamu wa Nigeria wanasema ujumbe wao 'ulifanikiwa'. Picha: ActuNiger

Waziri Mkuu alitaja vikwazo vya ECOWAS, ambavyo vimeanza kusababisha ugumu wa maisha, kuwa ''ukosefu wa haki'' na kwamba ni kinyume na sheria za jumuiya hiyo. Hata hivyo, alisema kuondolewa kwa vikwazo hivyo sio sharti la mazungumzo.

'Dhamira yenye mafanikio'

Kiongozi wa ujumbe wa wanazuoni hao wa Kiislamu, Sheikh Abdullahi Bala Lau, aliwaambia waandishi wa habari kwamba walikuwa nchini Niger kwa ''dhamira ya maridhiano.'' Alisema walimwambia kiongozi huyo wa kijeshi kuwa mazungumzo ni muhimu kutatua mgogoro huo.

Sheikh Lau alisema kabla ya safari yao ya Niger, walimweleza Rais wa Nigeria Bola Tinubu ambaye pia ni mkuu wa ECOWAS kwamba matumizi ya nguvu kugeuza mapinduzi hayafai.

Mwanazuoni huyo wa Kiislamu alisema dhamira yao kwa Niamey ''ilifanikiwa'' katika kurejelea kupata ahadi ya mazungumzo kutoka kwa junta. Hata hivyo, alisema hawakukutana na Rais aliyeondolewa madarakani Mohamed Bazoum kwa sababu haikuwa sehemu ya misheni yao.

Rais wa Nigeria Bola Tinubu, ambaye kwa sasa ni mwenyekiti wa jumuiya ya Afrika Magharibi ECOWAS, alikuwa ameidhinisha juhudi za upatanishi za viongozi hao wa kidini. Wanatarajiwa kumfahamisha kuhusu matokeo ya ziara yao.

Mahusiano ya kihistoria

Kabla ya wakoloni Waingereza na Wafaransa kuwagawanya katika karne ya 19, jamii za Niger na sehemu nyingi za Nigeria walikuwa watu moja, walioshiriki mifumo ya kidini, kitamaduni na lugha na kiutawala.

Uhusiano huu wa kihistoria na kuheshimiana umeendelea hadi sasa bila kujali historia yao ya kikoloni kwani watu wa Niger na kaskazini mwa Nigeria wengi wao ni Waislamu na wanaozungumza Kihausa. Hili ndilo jambo lililosisitizwa na viongozi wa Kiislamu katika ziara hiyo.

Hii inaonekana kama sehemu ya sababu kwa nini junta inakaribisha viongozi wa kimila na kidini kutoka Nigeria. Kabla ya ziara ya wanazuoni wa Kiislamu, kiongozi huyo wa kijeshi alikuwa amempokea mfalme wa Nigeria, Amiri wa zamani wa Kano, Muhammadu Sanusi II.

Rais aliyeondolewa madarakani Mohamed Bazoum anazuiliwa na jeshi la serikali tangu mapinduzi ya Julai 26. Kumekuwa na ongezeko la wito wa kuachiliwa kwake huku Umoja wa Afrika, Marekani na Umoja wa Mataifa zikieleza wasiwasi wake kuhusu hali yake.

Hadi sasa, viongozi hao wa mapinduzi wamesalia na msimamo mkali kutokana na shinikizo linaloongezeka la kutaka kuachia madaraka. Hiki kinaweza kuwa kigezo cha mvutano katika mazungumzo yoyote kati ya viongozi wa mapinduzi na ECOWAS.

TRT Afrika