Viongozi wa Afrika wametoa wito wa ushirikiano zaidi wa kikanda katika kupambana na ugaidi siku ya Jumatatu katika mkutano wa kilele wa kutafuta suluhu zinazoongozwa na Afrika kwa changamoto za kiusalama za bara hilo, ikiwa ni pamoja na kuunda jeshi la kikanda.
Kuanzia nchini Mali, wanamgambo wenye itikadi kali wamejiimarisha katika eneo la Sahel, wakienea kusini zaidi na kutishia mataifa ya pwani ya Afrika Magharibi huku makundi zaidi yakipigana katika Pembe ya Afrika, Ziwa Chad na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
"Kitovu cha ugaidi kimehama kutoka Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini na kuingia katika Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara iliyojikita zaidi Sahel," Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina Mohammed aliuambia mkutano wa kilele wa kukabiliana na ugaidi mjini Abuja.
"Hali hasa katika Sahel ni mbaya... eneo hilo sasa linachangia karibu nusu ya vifo vyote vinavyotokana na ugaidi duniani."
Kubadilishana taarifa
Rais wa Nigeria Bola Ahmed Tinubu aliungana na viongozi wenzake Rais wa Ghana Nana Akufo-Addo na Rais wa Togo Faure Gnassingbe kuhimiza ushirikiano zaidi wa kikanda, ushirikiano wa kijasusi na kufanya kazi ili kuunda kikosi cha jeshi.
"Kikosi kama hicho kinaweza kusimama kama kizuizi kikubwa kwa operesheni kubwa na za muda mrefu za kigaidi," Tinubu alisema.
Nchi kadhaa za Kiafrika tayari zinashirikiana katika kikosi kazi cha pamoja cha mataifa mbalimbali katika maeneo ya mpaka wa Ziwa Chad.
Gnassingbe wa Togo pia alitoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kufanya kazi nzuri zaidi katika kusaidia mataifa ya Afrika kufadhili operesheni zao za kukabiliana na ugaidi.
Miaka ya uhasama
Niger, Burkina Faso na Mali zimekumbwa na mzozo wa miaka mingi na makundi ya waasi. Mapinduzi katika yote matatu pia yametatiza ushirikiano wa kikanda.
Mwezi uliopita, Niger ilisema wanajeshi wake 23 waliuawa katika shambulio la "kigaidi" karibu na mpaka wa Burkina Faso na Mali katika eneo ambalo mashambulizi ya waasi ni ya kawaida.
Lakini ghasia zinazidi kuenea hadi kwenye mipaka ya pwani ya Ghuba ya Guinea, Ghana, Togo, Benin na Ivory Coast.
Kuondolewa kwa wanajeshi wa Ufaransa kutoka Sahel kumeongeza wasiwasi juu ya kuenea kwa ghasia.
Hofu kuu
Wasiwasi mmoja mkubwa ni mamilioni ya silaha ndogo ndogo mikononi mwa makundi yasiyo ya kiserikali katika bara hilo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Nigeria Yusuf Tuggar alisema.
Lakini alisema mataifa ya Afrika pia yanakabiliwa na changamoto mpya katika kupambana na waasi wanaopigana kama vile athari za hali ya hewa, kuvunjika kwa ushirikiano na baadhi ya mataifa, habari za uongo kwenye mitandao ya kijamii na uhamishaji wa fedha usiodhibitiwa.
"Leo changamoto ya kupambana na ugaidi ni tofauti kwa kiwango... Tunapambana na mitandao isiyojua mipaka," alisema.
"Afrika inajikuta iko katika vita ya kila mtu."