Na Lynne Wachira
TRT Afrika, Nairobi, Kenya
Waandalizi wa mbio za Valencia marathon wamekutanisha wanariadha hodari kwa Makala ya mwaka huu ambayo yatafanyika Jumapili.
Ushindani mkali unatarajiwa kati ya bingwa wa dunia na Olimpiki Joshua Cheptegei wa Uganda, Kenenisa Bekele wa Ethiopia, Alexander Mutiso wa Kenya na Gabriel Geay wa Tanzania.
Macho yote yameelekezwa kwa Joshua Cheptegei ambaye anashiriki mbio za marathon kwa mara ya kwanza kabisa. Cheptegei alitangaza nia yake ya kushiriki mbio za marathon baada ya kutetea taji lake la dunia la mita elfu kumi wakati wa mashindano ya dunia mjini Budapest mwezi Agosti.
Licha ya kuwa katika mbio za marathon kwa mara ya kwanza, Cheptegei si mgeni mjini Valencia kwani aliandikisha rekodi mpya ya dunia ya mbio za mita elfu kumi mjini humo mwaka wa 2020.
“Nina uhusiano wa karibu sana na mji wa Valencia, nina kumbukumbu nyingi nzuri kutoka hapa na ndiposa ilikuwa rahisi kufanya uamuzi kushiriki mbio hizi kama ufunguzi wa Maisha yangu katika marathon.” Alisema Cheptegei kutoka Valencia huku pia akizungumzia malengo yake.
“Ndoto yangu ni kukimbia muda wa kasi la labda kuvunja rekodi ya Taifa ya marathon, vile vile nina furaha nyingi kushiriki mbio hizi pamoja na Kenenisa Bekele ambaye nimemtazama kama mfano wa kuigwa tangu nikiwa shuleni.”
Cheptegei anashilia rekodi ya dunia katika mbio za mita elfu 5000 na za mita elfu kumi ambazo zilishikiliwa na Kenenisa Bekele, ni mashindano kati ya aliyebobea na anayebobea kwa sasa.
Katika upande wake Bekele mwenye umri wa 41 anajivunia kushiriki mbio na wanariadha wenye umri mdogo kumliko huku akiwa na matumaini kuwa weledi wao utampa msukumo zaidi na kumwezesha kuandikisha matokeo ya kujivunia.
“Hakuna mwanariadha ambaye atashikilia rekodi ya dunia milele, ni wazi kuwa wanariadha wachanga na walio na uwezo zaidi watajitosa ulingoni, ninajivunia kutangamana nao,” alisema Bekele.
Bekele ambaye anashiriki mashinadano kwa mara ya kwanza tangu kukatiza uhusiano wake na kampuni ya Nike atavalia jezi ya wadhamini wake wapya wa Kampuni ya vifaa vya michezo ya Anta. Alishiriki mashindano kwa mara ya mwisho mwezi Aprili mwaka huu ambapo alijiondoa baada ya kilomita ishirini za kwanza.
Cheptegei na Bekele watakabiliana na ushindani mkali kutoka kwa Gabriel Geay ambaye anarejea mjini Valencia baada ya kumaliza katika nafasi ya pili mwaka uliopita nyuma ya Kevin Kiptum ambaye sasa ni anashikilia rekodi ya dunia ya mbio za marathon.
Zaidi ya kumaliza katika nafasi ya pili Gaey aliandikisha rekodi mpya ya Tanzania (2:03:00) na kuandikisha historia kama mwanariadha wa kwanza kutoka Tanzania kukimbia mbio za marathon chini ya muda wa 2:04:00.
“Mji wa Valencia ni mji wa historia, ninaandikisha matokeo ya kufana wakati wote ninapokuja hapa hivyo basi ninatarajia jumapili ya kufana.”
Kwa Upande wa wanawake, Joan Chelimo wa Kenya atarejea kwa mara ya pili baada ya kushiriki Makala ya 2020 huku mji wa Valencia ukiwakaribisha Worknesh Degefa na Melat Kejeta kutoka Ethiopia kwa mara ya kwanza kabisa.