Kundi la mamluki la Wagner la Urusi litaendelea na operesheni nchini Mali na Jamhuri ya Afrika ya Kati licha ya kiongozi wake kufanya uasi mwishoni mwa juma.
Katika mahojiano Jumatatu na kituo cha habari cha RT, Waziri wa mambo ya nje Sergei Lavrov alisema kwamba wanachama wa Wagner "wanafanya kazi huko kama wakufunzi. Kazi hii, bila shaka, itaendelea."
Aliongeza kuwa uasi wa Wagner hautaathiri uhusiano wa Urusi na "ushirika na marafiki."
Lavrov pia alisema uasi wa mkuu wa Wagner Yevgeny Prigozhin hautabadilisha chochote katika uhusiano wa Urusi na washirika wake.
"Kumekuwa na simu nyingi (kutoka kwa washirika wa kigeni) kwa rais (Vladimir) Putin... kuelezea kuwa wanaunga mkono wao," alisema.
Uhusiano wa Urusi
Alipoulizwa ikiwa kunaweza kuwa na mabadiliko yoyote kwa uhusiano wa kimataifa wa Urusi kama matokeo, Lavrov alisema:
"Pamoja na washirika na marafiki, hapana. Kuhusu wengine, kusema ukweli, sijali. Uhusiano kati ya Magharibi na sisi umeharibiwa. "
Kiongozi wa kundi la Wagner mwishoni mwa juma alifanya uaasi ambayo yalipelekea msafara wa kivita ukielekea mji mkuu wa Urusi Moscow.
Aligeuza vikosi vyake baada ya rais wa Belarus Alexander Lukashenko kufanya makubaliano ya kumaliza hali hiyo.
Vikosi vya kundi la mamluki vimechukua nafasi kubwa katika kupambana na uasi wa muda mrefu katika nchi hizo mbili za Afrika.
Wasemaji wa serikali za Mali na Jamhuri ya Afrika ya Kati, walikataa kutoa maoni yao kuhusu uasi huo na jinsi unavyoweza kuathiri mikakati yao ya usalama dhidi ya makundi ya wapiganaji, shirika la habari la Reuters linaripoti.
Uhalifu wa Kivita
"Uwepo wa (Wagner) nchini Mali unafadhiliwa na Kremlin na kama Wagner ana msuguano na Kremlin ... kwa kawaida Mali itakabiliwa na madhara katika masuala ya usalama," mchambuzi wa kisiasa wa Mali Bassirou Doumbia aliiambia Reuters.
Umoja wa Mataifa na madola ya Magharibi yameshutumu vikosi vya Wagner kwa kufanya uhalifu wa kivita unaowezekana pamoja na vikosi vya Mali.
Serikali ya Mali na Urusi zimekanusha madai hayo.
Pia wameshutumiwa kwa kutumia maliasili nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, Mali na kwingineko kufadhili mapigano nchini Ukraine - madai ambayo Urusi inakataa.