Mgogoro nchini Niger, ambao rais wake alipinduliwa Julai 26, unazidisha hatari kwa mamilioni ya watoto, Shirika la watoto katika umoja wa Mataifa limesema.
"Hali ya sasa inatia wasiwasi mkubwa na inaongeza mzigo mkubwa kwa hali mbaya ya kibinadamu," Mwakilishi wa UNICEF wa Niger, Stefano Savi, alisema katika taarifa mwishoni mwa wiki.
"Kwa sasa, zaidi ya watoto milioni mbili wameathiriwa na janga hilo na wanahitaji sana msaada wa kibinadamu."
Hata kabla ya vurugu kutokea hivi karibuni, karibu watoto milioni 1.5 walio chini ya umri wa miaka mitano walitabiriwa kuwa na utapiamlo mwaka 2023, ripoti iliongeza.
Mgogoro wa Kisiasa
Niger imeorodheshwa miongoni mwa nchi zenye misukosuko na maskini zaidi duniani, mara nyingi zikiwa chini zaidi katika orodha ya Maendeleo ya Binadamu ya Umoja wa Mataifa, kwa kigezo cha ustawi.
Rais aliyechaguliwa kwa njia ya kidemokrasia nchini humo, Mohamed Bazoum, alipinduliwa Julai 26, na kusababisha kulaaniwa duniani kote na pia kuwekewa vikwazo vya kibiashara na majirani wa Niger.
UNICEF ilisema inaendelea kutoa msaada lakini inakabiliwa na vikwazo vinavyoongezeka.
Ilikuwa na wasiwasi kuhusu kupotea kwa umeme, ambayo ilikuwa muhimu kwa kuweka chanjo za watoto na vitu vingine katika barafu.
'Vifaa vya kuokoa maisha'
Pia ilionyesha wasiwasi wake kwa makontena 21 ya "vifaa vya kuokoa maisha" ambayo ilisema yalikuwa yamekwama kwenye mpaka wa Benin na bandari ya Benin ya Cotonou. Makontena mengine 29 ya Niger kwa sasa yapo baharini, yakiwa na chakula cha dharura na mabomba ya sindano.
"UNICEF inatoa wito kwa dharura kwa pande zote katika mgogoro huo kuhakikisha kuwa wafanyakazi wa kibinadamu na vifaa vinawafikia kwa usalama watoto na familia zilizo hatarini zaidi pale zinapohitajika haraka," alisema Savo.
"Pia tunaomba kwamba mipango muhimu ya kibinadamu ilindwe dhidi ya athari za vikwazo na kupunguzwa kwa ufadhili."