Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) limesajili Mbuga ya Kitaifa ya Milima ya Bale, Ethiopia kama eneo la urithi wa dunia.
Kulingana na Wizara ya Utalii ya Ethiopia, Milima ya Bale "ni kimbilio la kijani kibichi na wanyamapori tele, inayotoa mazingira ya kupendeza na mkusanyiko wa misitu ya kahawa ya mwituni. Inajivunia njia bora za safari kwa wale wanapenda kutembea na kukwea milima."
Hifadhi ya Kitaifa ipo katika ardhi yenye ukubwa wa takriban hekta 215,000.
"Tunasherehekea uzuri wa dunia na kujitolea kwetu kulinda hazina zake," Fitsum Arega Balozi wa Ethiopia nchini Canada amesema.
Hifadhi ya Kitaifa ya Milima ya Bale, iko kusini mashariki mwa Ethiopia kilomita 400 kutoka jiji kuu la Addis Ababa.
Mbuga hiyo, iliyoanzishwa mwaka wa 1962, ina maziwa, ardhi yenye rutuba, na mabaki ya volkeno yenye mandhari ya kuvutia, na kuifanya kuwa mojawapo ya maeneo bora ya utalii, kulingana na Wizara ya Utalii ya Ethiopia.
Hifadhi hiyo pia imejaliwa kuwa na aina kadhaa za mimea, wanyama, na ndege.
Mbuga ya Kitaifa ya Milima ya Bale ni kivutio cha pili cha watalii nchini Ethiopia kupewa hadhi ya urithi wa dunia katika kikao cha 45 kinachoendelea cha Kamati ya Urithi wa Dunia cha UNESCO. Siku ya Jumapili, UNESCO ilisajili Mazingira ya Gedeo Cultural Landscape ya Ethiopia kama urithi wa dunia. Kivutio hiki kinajumuisha msitu, ambao umelindwa kupitia vizazi.
Urithi huo pia unajulikana kwa kilimo chake cha tabaka nyingi, ambacho kimefanywa kwa karne nyingi na watu wa Gedeo ambao pia ni mfano wa maarifa yao asilia katika uhifadhi wa mfumo wa ikolojia na rutuba ya udongo, kulingana na Wizara ya Utalii ya Ethiopia.
Serikali ya Ethiopia imesema kusajiliwa kwa maeneo hayo mawili kama turathi za dunia na UNESCO kunatarajiwa kusaidia kuimarisha juhudi za kuendeleza utalii nchini Ethiopia.
Kwa jumla sasa Ethiopia ina maeneo 11 amabyo yameorodheswa na UNESCO kwenye orodha ya Urithi wa Dunia wa UNESCO .