Umoja wa Afrika imeamua kusimamisha mara moja ushiriki wa Jamhuri ya Niger kutoka kwa shughuli zake zote na mashirika na taasisi zake.
Hali hii itabaki hadi pale Niger itarudi katika utaratibu wa kikatiba nchini humo.
Niger imekuwa chini ya uongozi wa kijeshi tangu 26 Julai mwaka huu wakati wanajeshi walimuondoa kwa nguvu rais Mohamed Bazoum.
Baraza la amani na usalama la Umoja wa Afrika limetoa uamuzi wake katika taarifa.
"Baraza limewataka wanajeshi kuweka masilahi ya juu zaidi ya Niger na watu wake juu ya yote mengine na kurudi mara moja na bila masharti kwenye kambi yao," baraza hilo limesema katika taarifa.
Baraza la amani na usalama ambalo lina wanachama 15 wanne ambao wanatoka Afrika Magharibi lilikutana 14 Agosti mwaka huu kujadilli swala la Niger.
Mkutano huo ulikosa kufanya maafikiano yoyote kwasababu nchi hazikukubaliana kuhusu uamuzi wa jumuiya ya Afrika magharibi, ECOWAS kutuma wanajeshi Niger.
AU sasa imeomba wanajeshi Niger kurejesha uongozi kwa mamlaka ya kiraia.
Umoja wa Afrika unasema mabadiliko ya serikali kinyume na katiba, kwa hali yoyote ile, hayafai kuhalalishwa.
Kuhusu uamuzi wa jumuiya ya Afrika Magharibi ya ECOWAS kutuma wanajeshi Niger , Umoja wa Afrika umesema "inazingatia uamuzi wa ECOWAS" wa kupeleka kikosi cha Kudumu nchini Niger".
AU itafanya tathmini ya athari za kiuchumi, kijamii na kiusalama za kupeleka wanajeshi nchini Niger na kutoa taarifa kwa baraza.
Baraza la bara la amani na usalama pia imepinga vikali kuingia kwa mhusika yeyote au nchi yoyote nje ya bara katika masuala ya amani na usalama barani Afrika ikiwa ni pamoja na ushirikiano na makampuni binafsi ya kijeshi nchini barani.
Baraza hilo pia limeomba tume ya Umoja wa Afrika kuteua na kupeleka mwakilishi Mkuu ili kuendeleza juhudi za upatanishi za jumuiya ya Afrika Magharibi ya ECOWAS.
Lakini je, nchi kusimamishwa na Umoja wa Afrika ina maana gani ?
Kwa sasa Niger inaungana na Sudan, Mali, Burkina Faso na Guinea ambazo zimesimamishwa kwa muda kutoshiriki kwa maswala ya Umoja wa Afrika. Nchi hizi ziko nchini ya utawala wa kijeshi.
Inamaanisha nchi haitaalikwa tena katika shughuli za Umoja wa Afrika hadi irejeshe uongozi kwa raia.
Niger sasa haiwezi kuwa na haki ya kupiga kura kwa maswala yoyote ya kikanda, Pia serikali hii haiwezi kuruhusiwa kuandaa mikutano yoyote ya kibara.
Wawakilishi waliochaguliwa kuwakilisha Niger katika kamati mbali mbali za Umoja wa Afrika hawataweza tena kuhusika katika mikutano yoyote.
Muda wa mpito
Kiongozi wa kijeshi wa Niger Jenerali Abdourahmane Tiani amesema kuwa uchaguzi nchini humo utafanyika baada ya miaka mitatu, akisema nchi hiyo itaendeleza mchakato wa mpito ambao hautadumu.
"Matarajio yetu sio kunyang'anya mamlaka," Jenerali Abdourahamane Tchiani alisema katika hotuba yake kwenye televisheni. Muda wa mpito wa madaraka "hautazidi zaidi ya miaka mitatu", alisema tarehe 20 Agosti katika hotuba yake kwa televisheni.
Lakini jumuiya ya magharibi , ECOWAS, imekataa kauli hii.
"Mabadiliko ya miaka mitatu hayakubaliki," Abdel-Fatau Musah, kamishna wa siasa na usalama wa ECOWAS, aliiambia idhaa ya Al Jazeera katika matangazo ya mahojiano siku ya Jumatatu.
"Tunataka utaratibu wa kikatiba urejeshwe haraka iwezekanavyo."