Uchaguzi DRC 2023: Wakongo waendelea kupiga kura, wakiri baadhi ya vituo kuchelewa kuanza. zoezi kuendelea Alhamisi

Uchaguzi DRC 2023: Wakongo waendelea kupiga kura, wakiri baadhi ya vituo kuchelewa kuanza. zoezi kuendelea Alhamisi

Wakati upigaji kura uliendelea nchini DRC, Tume ya Uchaguzi nchini humo imesema, uchaguzi utakuwa huru na wa amani.
Denis Mukwege mgombea urais nchini DRC. Picha/TRT Afrika. 

Wananchi nchini DRC mapema leo hii wamerauka katika vituo mbalimbali kwa ajili ya kupiga kura na kuchagua viongozi watakaowaongoza katika kipindi vya miaka 5 ijayo.

Upigaji huo wa kura unajumuisha kuchagua viongozi kadhaa katika ngazi ya kitaifa, majimbo na madiwani. Jumla ya wagombea urais 26 wamejitokeza, kati ya hao, mmoja ni mwanamke.

Mkazi wa Kinshasa nchini DRC. Picha/TRT Afrika. 

Mapema hii leo, Martin Fayulu, ambae ni mgombea urais alijitokeza katika kituo chake cha kupiga kura, kilichopo katika shule ya Athenee De la Gombe na kutimiza wajibu wake. Kwa mujibu wa mwandishi wa TRT Afrika, anasema mgombea huyo alisubiri kwa muda kabla ya kuingia ndani na kupiga kura kutokana na rabsha iliyosababishwa na baadhi ya wapiga kura waliotaka kuingia na Fayulu. Hata hivyo, polisi waliingilia kati na kudhibiti hali hiyo.

Punde tu baada ya kumaliza kupiga kura, Fayulu aliongea na waandishi wa habari. "Kwa taarifa nilizopata kutoka majimboni ni kuwa kuna baadhi ya vituo hapa Kinshasa bado havijafunguliwa, na vilivyofunguliwa havina vifaa na vitendea kazi. Lakini kiujumla zoezi linakwenda vyema na salama. Nawataka wananchi waende vituoni wakapige kura.’'

Katika nyakati tofauti, Denis Mukwege, ambae pia ni mgombea urais katika taifa hilo lenye utajiri mkubwa wa madini, amejitokeza mapema katika kituo chake cha kupiga kura cha shule ya Athenee de la Gombe na kutimiza wajibu wake.

Moja ya vituo cha kupiga kura mjini Kinshasa nchini DRC. Picha/TRT Afrika. 

Uchaguzi wa mwaka huu pia, unahudhuriwa na waangalizi kutoka AU pamoja na SADC, hata hivyo, waangalizi kutoka Jumuia ya Afrika Mashariki, hawakupata fursa hiyo. Enoch Kavindele, ambae ni muangalizi kutoka nchini Zambia, anasema teknolojia iliyotumika ya kupigia kura, ni mpya, na kuongeza kusema, "Huo ndio mustakbali ya sasa."

"DRC ndio nchi pekee waliyokuwa nayo, hivyo nawashauri wajitokeze kwa wingi kuchagua viongozi wao," amesema Kavindele.

Kwa mujibu wa Tume Huru ya Uchaguzi nchini humo, CENI, jumla ya wapiga kura milioni 40 wamejiandikisha kupiga kura. Jiji la Kinshasa ndio linaongoza kwa idadi kubwa ya wapiga kura, ambao ni takriban milioni 5.

Kwa upande wao, baadhi ya wananchi waliojitokeza kupiga kura, wameonyesha shauku yao ya kutaka uchaguzi huo uishe kwa amani, huku wakisisiza viongozi watakaoingia madarakani wawe na moyo wa kuleta maendeleo kwa wananchi wa taifa hilo.

"Tofauti ya uchaguzi wa mwaka huu na mwaka uliopita, mwaka huu kila kitu kimekuwa sawa, nimefika na kupiga kura mara moja," anasema mkazi wa jijini la Kinshasa.

Kwa mara ya kwanza katika historia ya Congo, raia wake waishio ugenini wataweza kushiriki katika uchaguzi mkuu. Kwa hatua ya kwanza, raia kutoka nchi tano ndio watakaoweza kushiriki, ambazo ni, Marekani, Canada, Ubelgiji, Ufaransa na Afrika ya Kusini ambako wapiga kura 13600 walijiorodhesha.

Tume Huru ya Uchaguzi CENI imesema, itaongeza muda katika vituo ambavyo vimechelewa kufunguliwa na zoezi lakupiga kura kwa baadhi ya maeneo litaendelea kesho kutokana na sababu mbalimbali zilizotajwa na CENI ikiwa ni pamoja na ukosefu wa rasiliwatu.

TRT Afrika