Mauaji ya Ali Mohammed Kibao yameibua hisia kali nchini humo, huku taasisi mbalimbali za kutetea haki za binadamu zikitaka uchunguzi wa kina ufanyike/ Picha : wengine

Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kimesema kimesikitishwa na kinalaani kitendo cha utekaji na kuuawa kikatili kwa Ali Mohammed Kibao.

“TLS, inapenda kuvikumbusha vyombo vya dola juu ya majukumu yake kikatiba na kisheria ya kulinda watu na mali zao,” imesema sehemu ya Tamko lililotolewa na TLS na kusainiwa na rais wa Chama hicho Boniface Mwabukusi.

Kauli hii inakuja siku kadhaa baada ya taarifa za kutekwa kwa Ali Kibao na watu wasiojulikana akiwa ndani ya basi kutoka Tanga kuelekea jijini Dar es Salaam.

Hata hivyo, kwa mujibu wa uongozi wa Chadema, Kibao baadae alipatikana akiwa tayari ameuawa na mwili wake ukiwa na majeraha pamoja na dalili za kumwagiwa tingi kali.

Mauaji ya Kibao, yameibua hisia kali nchini humo, huku taasisi mbalimbali za kutetea haki za binadamu zikitaka uchunguzi wa kina ufanyike ili kubaini waliohusika.

Tayari TLS imetoa wito unaofanana na ule uliotolewa na Chadema wa kumtaka Rais wa nchi hiyo Samia Suluhu Hassan kuunda tume huru itakavyochunguza matukio ya kupotea, kutekwa na kuuawa kwa wananchi.

Wakati huo huo, TLS imetaka Waziri wa Mambo ya Ndani, IGP pamoja na Mkuu wa Mafunzo wa Jeshi la Polisi kuwajibishwa.

Tamko la TLS linaenda sambasamba na lile la Pamoja la Mabalozi wa Umoja wa Ulaya linalohimiza Serikali ya Tanzania kuhakikisha ulinzi wa upinzani.

“Tunatambua kwa wasiwasi mkubwa kwamba matukio haya ya hivi karibuni yanatishia misingi ya kidemokrasia na haki za wananchi wa Tanzania, katika nchi inayoheshimika kimataifa kwa amani na utulivu,” imesema sehemu ya Tamko hilo ambalo limesainiwa na balozo za nchi kadhaa ikiwemo Canada, Uingereza, Norway, Uswisi, na kuendelea.

Kwa upande wake, Rais Samia amelaani tukio hilo punde tu baada ya taarifa ya kifo cha Kibao kutangaza rasmi na Chadema, na kutaka vyombo vya dola kufanya uchunguzi haraka iwezekanavyo.

Hata hivyo, kilio kilichopo sasa hivi, ni cha kuunda tume huru itakayoongozwa na mahakimu kuchunguza mkasa huo.

Kibao ambae ni mkazi wa Mkoa wa Tanga, na kwa miaka mingi amekuwa akiishi jijini humo, kifo chake na mazingira aliyouawa yameleta simanzi. Baadhi ya wachambuzi wa kisiasa nchini humo, wanasema tukio hilo ni la aina yake na haliwajawahi kutokea kwa mtu kutekwa akiwa katika usafiri wa umma.

Jeshi la Polisi nchini Tanzania limetoa wito kwa yeyote mwenye taarifa kuhusiana na kifo cha aliyekuwa Mjumbe wa Sekretarieti ya CHADEMA Ally Mohamed Kibao, aziwasilishe ili kusaidia kufanikisha kukamilika mapema kwa tukio hilo.

Rais wa Tanzania Samia Suluhu naye amezitaka mamlaka za uchunguzi za nchi hiyo kumpelekea taarifa ya kina kuhusu tukio hilo na kwa haraka.

TRT Afrika