Aliyekuwa mgombea Urais katika kinyang'anyiro cha uongozi wa Chama Cha Mawakili Tanganyika (TLS), Wakili Sweetbert Nkuba ametangaza kupinga matokeo mahakamani yaliyompa ushindi Wakili Boniface Mwabukusi huku akitaja sababu mbalimbali anazodai zimehujumu uchaguzi huo.
"Sikubaliani na matokeo hayo na jambo la pili, nimejipinga kupinga matokeo kwani hayaakisi uchaguzi wenyewe," alisema Nkuba wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, Tanzania.
Kamati ya uchaguzi ya TLS ilimtangaza Mwabukusi kama Rais wa chama hicho baada ya kupata kura 1.274 ambazo ni sawa na asilimia 57.4, na hivyo kumshinda Sweetbert Nkuba na wagombea wengine, akiwemo Revocutus Kuuli, Ibrahim Bendera, Paul Kaunda na Emmanuel Muga katika uchaguzi uliofanyika Ijumaa, Agosti 2, 2024.
Hata hivyo, Nkuba amesisitiza kuwa mchakato huo ulitawaliwa na mizengwe, akiioneshea kidole cha lawama, kamati ya uchaguzi ya TLS.
"Kamati ya uchaguzi ilikuwa inajua idadi ya wapiga kura wakati inaandaa karatasi za kupigia kura, Lakini katika hali ya kushangaza na isiyo ya weledi, kamati iliishiwa karatasi za kupigia kura, hali iliyowalazimu kwenda kuchapisha karatasi zingine za kupigia kura...mnaweza kuona ni namna gani kamati ya uchaguzi ilivyokuwa haijajipanga ama kwa makusudi kuamua kuhujumu zoezi zima la uchaguzi huo," alidai Nkuba.
Kulingana na Nkuba, wakati mawakala wa uchaguzi walikatazwa kuingia na vifaa vya mawasiliano katika chumba cha kuhesabia kura, ilishangaza kuona matokeo kuanza kutangazwa kwenye mtandao wa X kabla matokeo rasmi hayajatangazwa na kamati.
"Tunaamini hizi ni hujuma za kamati ya uchaguzi na ni dhahiri kuwa kamati imekosa weledi na msimamo na imeshiriki kikamilifu katika kunajisi na kuhujumu mchakato mzima wa uchaguzi, kwa hiyo mimi napinga matokeo haya na ninakwenda mahakamani kupinga matokeo haya nikiamini kuwa matokeo haya yatafutwa na kuitishwa kwa uchaguzi mpya," aliongeza Nkuba.
Mwabukusi, ambaye hapo awali alienguliwa kuwania urais wa TLS kabla ya kukata rufaa mahakama kuu na kushinda, atakiongoza Chama hicho cha Mawakili kwa kipindi cha miaka mitatu.