tanzanian to be repatriated from Israel

Serikali ya Tanzania imesema imeandaa mpango wa kuwarejesha nchini Watanzania waliopo nchini Israel na maeneo mengine ya karibu.

Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi hiyo, ambapo imesema, hatua hiyo, inafuatia kuendelea kuzorota kwa hali ya usalama Israel na maeneo mengine ya jirani.

“Serikali imefikia uamuzi huo baada ya kufanya tathmini na kujiridhisha kwamba mazingira ya sasa yanaruhusu zoezi hilo kufanyika,” imesema taarifa hiyo ya Wizara, na kuwataka Watanzania walio tayari kurudi kujiandikisha katika ubalozi wa Tanzania uliopo Tel Avivi, Israel.

Taarifa hiyo haijataja idadi ya Watanzania waliopo nchini humo, lakini imesema watakaonufaika na mpango huo, ni wale waliopo katika maeneo mengine ya karibu. Mbali na watumishi katika ubalozi wa Tanzania mjini Tel Avivi, baadhi ya Watanzania pia wapo nchini humo kwa ajili ya masomo na shughuli nyengine mbalimbali.

Hatua hii inakuja baada ya wiki ya mashambulizi makali ya Israel dhidi ya Palestina, ambayo mpaka sasa yamesababisha vifo vya zaidi watoto mia saba huku maelfu wakiyakimbia makazi yao. Umoja wa Mataifa na jumuia ya kimataifa imeonya kutokea kwa janga la kibinadamu hasa baada ya Israel kusitisha huduma zote za kijamii ikiwemo maji na umeme hasa katika maeneo nyeti kama vile hospitali.

Tanzania, ni nchi ya kwanza katika eneo la Afrika ya Mashariki kuchukua uamuzi wa kurejesha nyumbani raia wake. Hii inaweza kuleta chachu kwa mataifa mengine nayo kuchukua hatua kama hii.

TRT Afrika