Bunge la Sudan Kusini limeidhinisha sheria mbili kuhusu utengenezaji wa mifumo ya haki na sheria.
Hii itafungua njia ya uwajibikaji na haki kwa waathiriwa wa dhulma zilizofanywa tangu kuanza kwa vita nchini humo Disemba 2013.
Mgogoro huo ni kati ya migogoro iliyowalazimu maelfu ya raia kuhama makazi yao.
Zaidi ya wakimbizi milioni 2.2 walisambaa katika nchi jirani za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Ethiopia, Kenya, Sudan na Uganda.
Lakini, vita katika nchi jirani ya Sudan tangu Aprili 2023 vimewalazimu maelfu waliokuwa wamekimbilia nchini Sudan kurudi nyumbani Sudan Kusini bila chochote.
Miswada hiyo iliyopitishwa mnamo Septemba 3, 2024, iliwasilishwa kwa kamati za bunge ambazo zitashughulikia masuala ambayo hayajakamilika na kufanya mabadiliko ya mwisho kabla ya kuipeleka kwa rais ili kutiwa saini.
Makubaliano ya amani kati ya seriklai ya Sudan Kusini na vikundi vya upinzani mwaka 2015 na 2018 kwa ajili ya kumaliza mzozo nchini Sudan Kusini yaliazimia kuunda vyombo vitatu vya kushughulikia dhulma zilizofanyika.
Miswada iliyo bungeni hivi sasa ni miwili kati yao.
Kwanza itaongoza kuundwa kwa Tume ya Ukweli, Upatanisho na pili ni Mamlaka ya Fidia.
Chombo cha tatu kinafaa kuwa mahakama ya mseto au 'hybrid court' ambayo itaundwa kwa ushirikiano na Umoja wa Afrika chini ya Mkataba wa 2015 wa Utatuzi wa Mzozo katika Jamhuri ya Sudan Kusini na Makubaliano ya Kuhuishwa ya 2018.
"Kuidhinisha kwa Sudan Kusini kwa miswada hii ya haki ya mpito iliyochelewa ni matokeo ya shinikizo endelevu kutoka kwa waathiriwa wa ukatili, familia zao, na mashirika ya kiraia," alisema Nyagoah Tut Pur, mtafiti wa Sudan Kusini katika Human Rights Watch.
"Lakini mengi zaidi yanasalia kufanywa ili kuhakikisha michakato ya kuaminika ya kuendeleza haki na kuzingatia haki za waathiriwa, haswa kuunda mahakama ya mseto."
Chini ya mswada wa sasa, Tume ya Haki na ukweli ina jukumu la "kuchunguza masuala yote ya ukiukwaji wa haki za binadamu, uvunjaji wa sheria na matumizi mabaya ya madaraka kupita kiasi" yanayofanywa na wahusika wote wa serikali na wasio wa serikali.
Tume ina mamlaka zaidi ya "kuchunguza, kuandika, na kutoa ripoti juu ya mwendo na sababu za migogoro" na "kupendekeza michakato ya waathiriwa kupata haki ikiwa ni pamoja na kupendekeza hatua za fidia."
Mkataba wa amani wa Sudan kusini wa 2018 unatoa fursa ya kuunda hazina na mamlaka ya fidia, kutokana na athari za mzozo huo kwa raia wa Sudan Kusini.
Lengo la mamlaka hiyo ni "kutoa msaada wa nyenzo na kifedha kwa raia ambao mali yao iliharibiwa na migogoro na kuwasaidia kujenga upya maisha yao."