Migrant helping Migrants/ TRT Afrika

Charles Mgbolu

Ilikuwani siku tulivu ya mwezi october tarehe 27 mwaka 2013 wakati ambao Sam Goncolo mwenye miaka 31 alianza safari mpaka Casablanca katika uwanja wa Mohammed V International Airport.

Sam alisafiri kilomita zaidi ya 2000 kutoka Monrovia mji mkuu wa Liberia kwenda kusoma kuhusu uhusiano wa kimataifa katika chuo cha Morocco.

Mpango wa Sam ulikua ni kuhamia Ulaya baada ya masomo.

Kama wahamiaji wengine, aliondoka nchini kwake akiwa na kiu kubwa ya kuachana na umasikini na kupata maisha ya ndoto zake.

Lakini watu wengi wanao safiri kutoka Liberia na mataifa mengine ya Afrika wamepotoshwa kuhusu njia ya kupata utajiri kwa haraka

Kwa upande wa Liberia habari potofu zinatokana na hali ya uchumi wa nchi hiyo katika kipindi ambacho nchi jaribu kuimarisha uchumi wake baada ya kukabiliana na vita mbili za wenyewe kwa wenyewe ambazo ziliikumba Liberia mwaka 1989 na mwaka 2003 na kusababisha vifo vya takribani watu 200,000.

Kwa mujibu wa taasisi ya kimataifa ya wahamiaji [IMO] zaidi ya raia wa Liberia 200000 wanaondoka katika nchi hiyo kila mwaka kwenda kutafuta maisha bora zaidi.

Kulikuwa na matarajio mengi nyumbani. Wazazi wangu ni maskini na hawafanyi kazi. Walikuwa wakinitegemea kufanya makubwa huko ulaya,” anakumbuka

Lakini baada ya kuhitimu kutoka chuo kikuu, Sam alikuwa na badiliko la moyo. Aliacha kabisa ndoto yake kubwa ya kwenda Ulaya na kurudi nyumbani Liberia. Pia aliwashawishi na kuwasaidia wahamiaji wengine kurejea katika nchi zao.

Dharura ya kimataifa

Azimio la Sam kusalia Morocco au kusafiri kuvuka Mediterania hadi Ulaya baada ya masomo yake lilianza kuyumba baada ya kuzungumza mara kadhaa na wahamiaji wa Kiafrika ambao wamekwama katika nchi hiyo ya Afrika Kaskazini.

Kufikia mwaka 2023, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi linasema, zaidi ya wahamiaji 22,000 kwa sasa wako nchini Morocco.

Kulingana na Benki ya Dunia, nchi sita za Kaskazini mwa Afrika - Algeria, Misri, Libya, Morocco, Sudan na Tunisia - kihistoria zimekuwa na zimesalia kuwa nchi muhimu kwa wahamiaji, usafiri na kuondoka kwenda Ulaya.

Kufikia katikati ya mwaka 2020, eneo dogo la Afrika Kaskazini lilikuwa na wahamiaji wanaokadiriwa kufikia milioni 3.2 wa kimataifa, karibu asilimia 61 wakiwa ni kutoka katika ukanda huo au katika nchi nyingine za Afrika.

"Niliguswa na hadithi za wahamiaji hawa na safari ngumu ambazo wamepitia. Niliona vijana wadogo wenye talanta nyingi ambao walikuwa na mengi ya kuyafanya kwa nchi zao lakini wameteseka sana kwenye safari ya hatari zaidi… na yote kwa nini?" Sam anaiambia TRT Afrika.

Safari ya kukatisha tamaa

Mnamo mwaka wa 2017, Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) liliripoti kuwa takribani wahamiaji 40 walikufa kwa kiu kaskazini mwa Niger baada ya gari lao kuharibika wakati wa jaribio la kufika Ulaya kupitia Libya. Maafisa wa Niger walisema watoto wachanga na wanawake ni miongoni mwa wahamiaji 44 waliokutwa wamefariki.

IOM iliripoti tena mnamo Desemba 2022 kwamba zaidi ya watu 5,600 wamekufa au kutoweka wakijaribu kuvuka Jangwa la Sahara katika kipindi cha miaka minane iliyopita, huku vifo vya wahamiaji 110 vikirekodiwa nchini Chad.

Na Aprili 2022, UN iliripoti kwamba zaidi ya watu 3,000 walikufa au kutoweka walipokuwa wakijaribu kuvuka Bahari ya Mediterania na Atlantiki, wakitarajia kufika Ulaya.

"Nilikuwa nimeona hali za wahamiaji. Wengi hawakuwa na makao na walilala nje kwenye joto au baridi. Wengi wao waliokuwa na watoto walikuwa wagonjwa. Niliwasiliana nao, na wengi wao walikuwa vijana na wenye vipaji. Wengi walikuwa na mawazo mazuri sana ya biashara. Walikuwa na kila kitu ambacho kingewasaidia kufanikiwa katika nchi zao.

"Lakini walikuwa wamepewa taarifa zisizo sahihi na walianza safari hii ambayo haikuwa kama walivyo ambiwa. Niliazimia kufanya kazi sasa ili kuwarudisha kwenye njia sahihi, na hii huanza na wao kurejea nyumbani.”

Kuzaliwa kwa binti wa Sam kulifanya azimio lake la kurudi Liberia kuwa thabiti zaidi.

"Niligundua kuwa baada ya kuhitimu kwangu, ikiwa ningesafiri kwenda Ulaya, ningekuwa kama mmoja wa wahamiaji hawa, nikiingia kwenye njia hatari na kuishia bila makazi kwa sababu sina hati sahihi. Sikuweza kufikiria kumweka mtoto wangu katika hali mbaya kama hiyo."

Kulingana na takwimu kutoka UNICEF, idadi ya watoto wahamiaji iliongezeka kwa asilimia 50 kutoka karibu milioni 24 mwaka 1990-2000 hadi milioni 36 mwaka 2020.

UNICEF pia inakadiria kuwa zaidi ya mtoto mmoja hufa kila siku kwenye njia hatari ya Mediterania ya Kati kutoka Afrika Kaskazini kwenda Italia. Kwa ujumla, zaidi ya vifo 29,000 vya wahamiaji vimerekodiwa kwa mwaka 2021, kulingana na Shirika la Kimataifa la Uhamiaji.

Kingsley Okoye, mwanasheria wa Uhamiaji katika nchi ya Afrika Magharibi ya Nigeria, anaiambia TRT Afrika, "Wengi wanalazimika kuondoka kwa sababu ya hali mbaya ya kiuchumi na wakati mwingine hali ya kisiasa katika nchi zao."

Nigeria imeshuhudia takriban raia milioni 1.7 wakihama katika mwaka 2020 pekee, kulingana na Idara ya Masuala ya Kiuchumi na Kijamii ya Umoja wa Mataifa.

"Baadhi ya vijana hawa huuza kila kitu walichonacho ili kulipia tiketi za ndege, wakitumai kufanya makubwa huko," Kingsley anaongeza.

Simulizi ya Sam inathibitisha hili.

"Nilikuwa nimewekeza pesa nyingi katika safari yangu. Niliuza kila kitu. Ndio maana kurudi nyumbani ulikuwa uamuzi mgumu sana kufanya. Kuachana na ndoto hii na kuwakabili wazazi wangu maskini, ambao walikuwa wanatarajia mengi kutoka kwangu. Nilijua wange sononeka sana moyoni,” Sam anasema.

Masomo ya Sam yalipokaribia mwaka wa mwisho, alikimbia kusaidia wahamiaji wengi waliokwama.

"Niliwaambia, nilikuwa na ndoto kama wao kwenda Ulaya, lakini ni kujiua kujaribu kuingia kwa gharama yoyote bila nyaraka sahihi."

"Ilikuwa vigumu kuwashawishi baadhi ya wahamiaji kufanya uamuzi wa kurejea nyumbani. Wengi walisema hawataweza kutazama familia zao usoni watakufa kutokana na aibu”

Lakini Sam aliendelea kurudi kwa wahamiaji na kufanya warsha kadhaa za uhamasishaji. Alifanya kazi na mashirika mengi ya misaada na kusaidia katika tafsiri za Kifaransa. Pia kulikuwa na vikwazo vingi vya kisheria.

“Niliandaa barua za maombi ya ufadhili na kuwezesha mikutano kadhaa na mashirika ya kimataifa ya misaada. Mikutano hii ilisaidia kuharakisha mchakato wa uchunguzi wa baadhi ya wahamiaji na hatimaye kuwarejesha makwao.”

Katika kushughulika mchakato wa kisheria, Sam anasema, kozi yake kuhusu mahusiano ya kimataifa "ilikuja vizuri sana".

Uso kwa uso na ukweli

Lakini baada ya kumaliza masomo yake, ulifika wakati wa Sam kukutana na familia yake.

"Usiku wa kabla ya kusafiri, sikuweza kulala. Ilikuwa Aprili 2021 nilirudi nyumbani Liberia pamoja na binti yangu, ambaye wakati huo alikuwa na umri wa miaka mitatu.”

"Kulikuwa na mshtuko na hali ya kutoamini kutoka kwa watu wanao nijua. Wazazi na marafiki zangu waliendelea kuniuliza ‘kwa nini?’ Walikuwa na matarajio mengi sana. Kwamba ningerudi mtu tajiri sana. Niliweza kujua wazi jinsi walivyokata tamaa”

Familia ya karibu ya Sam ilikubali uamuzi wake upesi, lakini aliendelea kutengwa katika hafla kubwa za familia, haswa na washiriki wengine wa familia yake kubwa.

"Kulikuwa na hali ya kutengwa. Hawakuwa na haja ya kusema. Nilihisi tu. Ilihuzunisha sana, hasa nilipojitahidi kumtunza binti yangu, ambaye aliugua muda mfupi baada ya kuwasili kwa sababu ya mabadiliko ya hali ya hewa na mazingira. Nilihitaji kuomba pesa kutoka kwa familia yangu, lakini sikujua ningemgeukia nani ili kupata usaidizi”

Kukutana kwa bahati

Lakini baada ya muda mfupi maisha ya kaanza kumwendea sawa.

Miezi michache baada ya kurejea kwake, IOM nchini Liberia ilimuunganisha Sam na Mpango wa Uponyaji nchini Liberia, ambako alifanyiwa ushauri nasaha na kupewa msaada wa kisaikolojia.

Sasa anafanya kazi kama mshauri katika mpango huo na kusaidia kuunganisha wahamiaji ambao wamefika ng'ambo, akisaidia kuwaunganisha na maafisa wa IOM katika nchi ambazo wamekwama.

"Nilipoteza kabisa imani na nguvu ya kujiamini kwangu baada ya kurudi. Lakini sasa nina furaha hadithi yangu imebadilika.”

Mpango wa kutoa msaada wa kisaikolojia na ushauri unafanya kazi nchini Liberia, wanazungumza kwenye redio na mara kwa mara kutoa vipeperushi vinavyoonya watu juu ya hatari ya uhamiaji haramu.

Mchungaji Philip Nushan, anayeongoza Mradi wa Ukweli na Maridhiano, anaiambia TRT Afrika, "Inaweza kuwa vigumu kuwarekebisha wahamiaji wanaorejea ambao tayari wamevunjika moyo."

"Hii inakuwa mbaya zaidi baada ya kukataliwa na jamii. Wanatazamwa kama walioshindwa. Wengi hujaribu kujiua na lazima wawekwe kwenye uangalizi mkali. Jamii yetu lazima ijifunze kusamehe zaidi,” anasema.

Mchungaji Nushan na timu yake katika taasisi hiyo wanafanya kazi na wanasaikolojia ya kuunda programu ya kina ambayo inawafunza wahamiaji wanaorejea kuhusu ujuzi wa kazi ambao unaweza kuwasaidia kupata ajira.

“Tunashtuka tunaposikia familia zao zikiwasemea matusi usoni. Tunajaribu kuwa familia yao mpya, na hii imewasaidia wengi wao kupona”

Sam anasema maisha yake sasa yamerudi kwenye mkondo. Hivi majuzi alimaliza kozi mbili za diploma katika usimamizi wa hoteli na utalii na usimamizi wa huduma kwa wateja.

"Ni kwa sababu nina imani kubwa na nchi yangu na kile inachoweza kutoa ulimwengu. Ninaamini kwamba siku moja ulimwengu utakuja mbio kuzuru Liberia, na nitakuwa hapa… tayari na kwa subira.”

TRT Afrika