Kauli mbiu ya mwaka huu ya kuadhimisha siku ya kuzuia kujiua ni 'Kujenga Tumaini kupitia Vitendo./ Picha : Reuters

Visa vya watu kujitoa uhai vimeendelea kuongoezeka, huku takwimu ikionyesha kuwa zaidi ya watu 800,000 hujiua kila mwaka kote duniani.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya duniani, kujiua ni ya pili katika kusababisha vifo vingi zaidi miongoni mwa vijana kati ya miaka 15-29.

''Kujiua kulikuwa sababu ya pili kuu ya vifo kati ya wasichana (baada ya hali ya uzazi) na sababu ya tatu ya vifo vya wavulana (baada ya ajali na vurugu kati ya watu,'' ilisema taarifa ya WHO.

Japo kujiua kumehusishwa kwa kiasi kikubwa na magonjwa ya afya ya akili, bado visa vingi vinakuwa na kiini cha ndani kama kichochezi.

Wataalamu wa afya nchini Tanzania wanaeleza kuwa hali mbaya ya uchumi imewasukuma wengi waliojiua au kujaribu kujiua.

''Tafiti zetu tu za magonjwa ya Afya ya Akili, zinaonysha kuwa magonjwa ya akili yanachangia kwa kiasi kikubwa katika kupelekea hali ya kujiua,'' anasema Dkt Godwin , daktari Bingwa wa wa Afya ya Akili Tanzania.

''Lakini magonjwa ya akili vile vile yanahusiana sana na umaskini. Kwa hiyo hali ngumu ya maisha inawezekana ikapelekea hali ya kujiua kwasababu watu walio na ugumu wa maisha wanasemekana kuwa na magonjwa ya akili.'' ameongeza Dkt Godwin.

Tarehe 10 Septemba kila mwaka imetengwa kama siku ya kuzingatia kuzuia kujiua, ambapo inalenga kupunguza unyanyapaa na kuongeza uelewa miongoni mwa mashirika, serikali, na umma, na kutoa ujumbe wa kipekee kwamba kujiua kunaweza kuzuilika.

Licha ya maendeleo aliyopatikana katika miaka chache ya nyuma, bado takwimu za wanaojiua zinaogofya. kwa mujibu wa Shirika la Afya duniani WHO, mtu mmoja hufa kila sekunde 40 kutokana na kujiua.

“Kila kifo ni msiba kwa familia, marafiki na wafanyakazi wenzake. Hata hivyo kujiua kunaweza kuzuilika.'' amesema Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt Tedros Adhanom Ghebreyesus

''Tunatoa wito kwa nchi zote kujumuisha mikakati iliyothibitishwa ya kuzuia kujiua katika programu za kitaifa za afya na elimu kwa njia endelevu,'' alionmgeza Dkt Tedros.

Nchini Tanzania, hakuna takwimu za kuonyesha idadi ya watu wanaojiua kila mwaka. Lakini Dkt Godwin, anasema taarifa zilizoko katika vyombo vya habari na ripoti chache wanazopokea, zinaonyesha vifo hivo vimeongezeka katika miaka ya karibuni.

''Kwa Tanzania, tatizo nalo ni kubwa. Ukiangalia tu ule ushahidi wa kimazingira utaona kwamba kun ahabari nyingi sana kwa sasa hivi watu wanajiua. Sasa vile ni viashiria kwamba hili tatizo lipo na lipo kwenye jamii na linaendelea,'' Dkt Godwin ameambia TRT Afrika.

Sababu kuu za kujiua

Sonona: Hali ya kupatwa na huzuni kubwa wakati jambo linatokea, kama vile kifo, au kupoteza ajira au hasara kubwa katika biashara.

Utumiaji wa dawa za kulvya : Huu ni utumiaji usiokuwa na mipaka na kusababisha uraibu na hatimaye mtu kushindwa kudhibiti hisia zake. Watu walioathirika na uraibu wa dawa za kulevya mara nyingi wanakosa kujielewa au kujua wanachokifanya namara nyingi huishia na ugonjwa wa akili.

Magonjwa ya Akili:

Suluhisho la msingi lipo katika jamii

Mingi ya sababu zinazopelekea watu kujiua au kutaka kujiua zinaweza kuepukika. Wataalamu wanasisitiza kutambuliwa kwa vichochezi za hisia hizo na kuangazia namna ya kuziondoa.

''Msingi wa utatuzi wa tatizo la kujiua unatokea kwenye jamii,'' anasema Dkt Godwin. '' Jamii inabidi ielimishwe zaidi kuhusu haya masuala ya kujiua lakini elimu ya afya ya akili kwa jumla inatakiwa itoke kwa wataalamu kwenye mahospitali iwafikie jamii iweze kuelewa ni njia gani za kutatua hili tatizo na njia ya kuzuia,'' anaongezea daktari huyo bingwa.

Kuzuia au kupunguza utumiaji wa dawa za kulevya pia kunasaidia kuepuka matatizo haya ya kutaka kujiua.

''Hii inatakiwa ianzie kwa wazazi kuwalinda watoto wao manyumbani. Kwasababu dawa za kulevya zimeonyesha pia zinachangia sana katika kusababisha watu kutaka kujiua. Na dawa za kulevya izi ikijumuishwa na pombe. Kwa hiyo matumizi ya pombe yakiweza kuhumizwa yapungue inaweza kusaidia sana kupunguza tatizo la kujiua,'' Dkt Godwin anaendelea kuambia TRT Afrika.

Wataalamu pia wansema njia bora ya kupnguza visa hivi ni kuimarisha matibabu ya afya ya akili katika ngazi zote. Hii ni kwasababu Afya ya Akili inaendelea kuwa sababu kubwa ya watu kutaka kujiua duniani.

Takwimu za WHO zimeonesha pia kuwa nchi zilizoendelea zimekuwa na idadi kubwa ya watu wanaojiua au kuataka kujiua. Wataalamu wanasema huenda ikawa ni kutokana na kiasi kikubwa ya magonjwa yasiyoambukiza na mtindo wa maisha.

Pia takwimu hizo zimeonesha kuwa wanaume wana hatari mara tatu zaidi ya wanawake.

Kauli mbiu ya mwaka huu ya kuadhimisha siku ya kuzuia kujiua ni 'Kujenga Tumaini kupitia Vitendo.'

TRT Afrika