Leo ni siku 500 tangu Sudan ianze kushuhudia mzozo mbaya zaidi wa kibinadamu kuwahi kutokea.
Mashirika ya kimataifa ya misaada ya kibinadamu yanasema huu ni wakati mgumu kwao kwani kwa zaidi ya miezi 16 wameshindwa kutoa msaada wa kutosha kwa mahitaji ya matibabu yanayoongezeka nchini, kuanzia janga la utapiamlo kwa watoto hadi milipuko ya magonjwa.
"Leo watoto wanakufa kwa utapiamlo kote Sudan. Msaada wanaohitaji kwa haraka sana haujafika na, inapotokea, mara nyingi unazuiwa,” anasema Tuna Turkmen, Mratibu wa Dharura wa MSF huko Darfur.
Mapigano kati ya Vikosi vya Rapid Support Forces (RSF) na Vikosi vya Wanajeshi wa Sudan (SAF), kuanzia mji mkuu Khartoum Aprili 15, 2023, yamekuwa yakiendelea katika maeneo mengi ya nchi, na kusababisha mgogoro wa kibinadamu ambao haujawahi kushuhudiwa nchini Sudan.
"Vikwazo vizito kutoka pande zote mbili zinazopigana vina uwezo mdogo sana, ikiwa ni pamoja na kutoa misaada," inasema Médecins Sans Frontières (MSF).
Mzozo huo umesababisha makumi ya maelfu ya watu kuuawa na kujeruhiwa. Kati ya Aprili 2023 na Juni 2024, Shirika la MSF linasema lilitibu majeruhi 11,985 wa vita katika hospitali zinazosaidiwa.
Vurugu hizo zimesababisha mzozo mkubwa zaidi wa wakimbizi duniani. Umoja wa Mataifa unasema zaidi ya watu milioni 10, au mtu mmoja kati ya watano nchini Sudan, wamelazimika kukimbia makazi yao, wengi wao wakikabiliwa na kuhama mara kwa mara.
Wataalamu wanasema utapiamlo unaongezeka huku kukiwa na ongezeko la bei za vyakula na ukosefu wa vifaa vya kibinadamu.
Zaidi ya hali ya janga katika kambi ya Zamzam ya Darfur Kaskazini, vituo vya kulisha wagonjwa wa ndani vya MSF katika maeneo mengine ya Darfur kama El Geneina, Nyala na Rokero vimeripotiwa kujaa wagonjwa.
"Kusini mwa Khartoum, MSF imezuiwa kuleta vifaa vya matibabu na wafanyakazi wa kimataifa katika hospitali kwa miezi mingi. Inazidi kuwa vigumu kutoa huduma za matibabu zinazohitajika kwa wagonjwa wetu, hata kwa huduma za dharura,” alisema Claire San Filippo, Mratibu wa Dharura wa MSF nchini Sudan.
"Mnamo Julai, kwa mfano, malori yenye vifaa vya MSF katika maeneo mawili tofauti huko Darfur yalizuiwa kufika yanakoenda. Malori mawili yalishikiliwa na kikundi cha RSF, na moja lilikamatwa na watu wasiojulikana wenye silaha.” Claire ameongezea.
Suluhu za kisiasa za mzozo zinadorora huku pande mbili zinazozozana zikikosa kukubaliana mfumo wa maongezi ya amani.