Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika limetoa wito wa kusitishwa kwa mapigano mara moja bila masharti nchini Sudan.
Mgogoro wa kuwania madaraka kati ya vikosi vya jeshi la Sudan na kundi la wanamgambo wa Rapid Support Forces, RSF, pamoja na vikosi mbali mbali umeripotiwa kusababisha vifo vya watu 50 na wengi kujeruhiwa.
Mapigano yanaendelea kuripotiwa katika mji mkuu Khartoum tangu Jumamosi.
Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika limeitaja hali hiyo kuwa "mapigano ya mauaji."
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na AU baraza hilo "linadai Vikosi vya Wanajeshi wa Sudan na Vikosi vya RSF kutafuta suluhisho la amani kwa haraka na mazungumzo ya pamoja kama njia ya kukuza utulivu na kuheshimu matakwa ya watu wa Sudan kwa kurejesha demokrasia, katiba, utawala wa sheria na uhuru.”
Taarifa zaidi inasema, "Baraza litafanya misheni nchini Sudan ili kuwasiliana na washikadau wote wa Sudan kuhusu hali nchini humo."
Mkutano huo uliofanyika katika Tume ya Umoja wa Afrika mjini Addis Ababa, Ethiopia imesisitiza kuwa inasimama upande wa watu wa Sudan katika harakati zao za kupata serikali inayoongozwa na raia.
Mamlaka ya Kiserikali ya Maendeleo IGAD, pia ilifanya mkutano wa dharura wa mtandaoni, Jumapili.
Muungano wa IGAD
Sudan ni mwanachama wa kambi ya kikanda yenye nchi za Djibouti, Kenya, Ethiopia, Somalia, Sudan Kusini na Uganda.
Kupitia akaunti yake ya twitter, Katibu Mtendaji wa IGAD Workeneh Gebeyu anasema wakuu wa nchi "wamekubaliana kwa kauli moja kushiriki kutawanya hali hiyo kama jambo la dharura,"
Umoja wa Afrika na kambi ya kikanda IGAD wamekubali kubaki na msimamo mmoja kwa suala hilo.