Vifaa vya kupigia kura na wasimamizi wa uchaguzi wamefika katika vituo vya kupigia kura kote nchini Sierra Leone tayari kwa uchaguzi mkuu wa tano nchini humo tangu kumalizika kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe 2002.
Zaidi ya wapiga kura milioni tatu watamchagua rais wa nchi hiyo kutoka kwa wagombea 13, wakiwemo wagombea wakuu, rais wa sasa Julius Maada Bio na Samura Kamara.
Matokeo ya kinyang'anyiro cha urais yanatarajiwa kutangazwa siku chache baada ya kupiga kura.
Iwapo hakuna mgombea yeyote wa urais atakayepata angalau 55% ya kura katika duru ya kwanza, duru ya pili itafanyika katika muda wa wiki mbili.
Tume ya Uchaguzi ya Sierra Leone ilisema matokeo yatatumwa kwa njia ya kielektroniki na kwa njia ya moja kwa moja na mchakato wa kuhesabu na kujumisha kura utafanywa katika ngazi ya kikanda.